MWANZA: Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Kituo cha Ukiriguru mkoani Mwanza imetakiwa kufanya utafiti unaoendana na hali halisi ya matokeo ya upatikanaji wa mazao kwa wakulima hatua itakayosaidia kuwa na kilimo chenye tija pamoja na kuinua uchumi wa mkulima na kuongeza pato la taifa kwa ujumla .
Akizungumza na na watumishi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Ukiriguru mkoani Mwanza katika ziara yake ya kikazi Januari 10,2024 Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde amesema kuwa utafiti unaonesha kuwa mbegu ya UK 08 inaweza kuzalisha kilo kati ya 1000 hadi 1200 kwenye heka moja lakini ikienda kwa mkulima wa kawaida anapata chini ya kilo 500 kwa heka moja hivyo kupelekea matokeo ya utafiti na uhalisia kukinzana.
“Wizara ipo tayari kushikamkono kila jitihada nzuri ambazo nyie mnazifanya ikiwemo kuwapa vitendea kazi vyote kama,hivi sasa unaniambia changamoto kubwa ni ya umwagiliaji waziri mie kaniambia sisi kama wizara sasa hivi tupo tayari kuwawekea mradi wa umwagiliaji ili TARI mzalishe mbegu katika mwaka mzima”…Alisema
Aidha katika hatua nyingine Silinde ameongeza kuwa Wizara ya Kilimo pamoja na Wizara ya Ujenzi wamekubaliana kwenye maeneo yote ya changamoto za barabara wanapojenga madaraja makubwa ambapo kunakuwa na upitishaji mkubwa wa maji watakapokua wanafanya kazi hizo Wizara ya Kilimo itakua sehemu ya hilo jukumu kwa kuhakikisha maji yanayotumika katika eneo la mradi hayapotei.
“Sisi tutakwenda kutengeneza mabwawa ambayo yatatumika kwa shughuli za kilimo tunatengeneza mipango endelevu ambayo itasaidia barabara zisiharibike lakini pia itaongeza shughuli nyingine za kilimo sisi tuna maji mengi sana yanayopotea kwa sababu tu ni maji yanayopita sasa hiyo ndio mipango endelevu ambayo Dk Samia Suluhu Hassan ametuagiza tuitekeleze”…Alisema
Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Ukiriguru ,Dk Paul Saidia amesema hadi sasa wana mbegu takribani 10 lakini pamoja na mbegu zote hizo wanachangamoto mpya iliyoibuka ya wadudu wasumbufu wafyonzao (chawajani) ambao wanafanya uharibifu kwenye mazao.
Naye mtafiti mgunduzi wa mbegu za Pamba kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Ukiriguru, Seperatus Kamuntu amesema kuwa kwa sasa mbegu ya UK 08 ndio iko kwenye soko na inazaa vizuri pia ina uvumilivu mdogo wa vishambulizi visumbufu.