TARI wafanikiwa kumdhibiti Tembo Mkonge

TAASISI ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), imefanikiwa kumdhibiti mdudu mharibifu katika zao la mkonge ajulikanaye kama Tembo Mkonge baada ya kufanya utafiti ndani ya miaka mitatu.

Mtafiti kutoka Kituo cha TARI Mlingano, Dk Mgaya Maumba amesema hayo wakati akizungumza na HabariLEO kuhusu mdudu huyo ambaye husababisha upotevu wa mimea katika shamba kwa asilimia 60.

Dk Maumba amesema majaribio ya kwanza ya utafiti wa mdudu huyo waliyafanya ndani ya kituo, kisha mwaka jana kutoka nje ya kituo na kufanya majaribio kwenye baadhi ya mashamba ya wakulima ambapo matokeo kwa asilimia 90 wamefanikiwa.

“Huyu mdudu ni mharibifu sana huwa anakula katikati ya kile kiini kichanga majani yanapokua, kwa hiyo majani yakiwa yanazaliwa yanatoka tayari yakiwa yameathirika.

“Huwezi kupata  nyuzi zilizokuwa nzuri za daraja la kwanza au daraja la pili, na wakati mwingine mkonge unakufa kabisa. Tunakamilisha tu taratibu tuweze kuifanya ile teknolojia sasa iwe rasmi,” amesema.

Kwa upande mwingine alisema kituo hicho cha Mlingano kimepanga kuzalisha mbegu katika maeneo ya wakulima, ili kuwapunguzia gharama za kusafiri umbali mrefu.

Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitatu, alisema kumekuwepo na mapinduzi makubwa katika uzalishaji wa mbegu za zao hilo.

“Tangu mwaka 2020/21 mpaka 22/23 TARI Mlingano  tumezalisha miche karibia milioni 12, ambapo mpaka mwaka huu Juni 30, miche 7,500,000 imesambazwa kwa wakulima.

“Kwa miche hiyo 7,500,000 ni sawa na ekari 4,687.5 zinazokwenda kupandwa miche hii au hekta 1875 ,” amesema.

Amesema kwa mbegu bora wakulima wakifuata kanuni bora za kilimo, matarajio ni kuvuna tani tatu za nyuzi kwa hekta moja kwa mwaka.

“Sasa kwa hekta hizi 1,875 katika mavuno ya wastani wa tani  tatu kwa kila hekta tunategemea jumla ya tani 5,625 zitakuwa zimevunwa ifikapo mwishoni mwa mwaka wa 2024/25.

Habari Zifananazo

Back to top button