DODOMA: Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Dk Thomas Bwana amehimiza matumizi ya teknolojia za kilimo zenye kuhifadhi mazingira na uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa tija.
Dk Bwana amehimiza hayo katika maadhimisho ya siku ya Mazingira Duniani yanayofanyika kitaifa Jijini Dodoma kuanzia Juni mosi hadi sita, 2024, yenye kauli mbiu ya ‘Urejeshwaji wa Ardhi, Ustahimilivu wa Hali ya Jangwa na Ukame’.
Amesema kilimo hakiwezi kutenganishwa na mazingira suala ambalo TARI kama taasisi yenye jukumu la kutekeleza utafiti wa kilimo kwa Tanzania Bara inazingatia ubunifu wa teknolojia za kilimo zenye kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi huku tija kwa mkulima ikiwa inapatikana.
Ametaja miongoni mwa teknolojia hizo kuwa ni mbegu za mazao mbalimbali zenye kustahimili ukame zikiwa zinatoa mavuno mengi na mbegu zenye sifa za kukomaa kwa muda mfupi hivyo wakulima kujipatia tija ya mavuno, kipato na kujikwamua kutokana na mvua za kusuasua na wakati mwingine kunyesha bila kutarajiwa.
SOMA: TARI Ukiriguru watakiwa kufanya tafiti zenye uhalisia
”TARI tuna mbegu ambazo zinastawi kwa muda mfupi na mavuno yanakua ni mengi hizi zote tunawapelekea wakulima mfano ni mbegu za mpunga aina ya NERICA zinazostawi maeneo yenye miiniko na zinavumilia ukame,” amesema.
Pia amesema kwa kutumia teknolojia ya makinga maji ina faida mbalimbali ikiwemo kuzuia mmomonyoko wa udongo, kuzuia upotevu wa rutuba ya udongo, kuvuna maji ya mvua shambani na inahifadhi unyevu shambani.
Teknolojia nyingine ni kitalu mkeka cha mpunga ambacho kinatumia maji na mbegu kidogo ambacho mkulima anaweza kukiandaa hata nyumbani kwake tofauti na ilivyo kawaida kuwa kitalu kinaandaliwa shambani.
Sambamba na Kitalu Mkeka, kilimo shadidi cha mpunga Dk Bwana anaitaja kuwa teknolojia rafiki ya kutunza mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwakuwa inahitaji maji kidogo shambani huku mavuno yakiwa mengi na hivyo maji mengine kutumiwa katika shughuli nyingine.
Kutokana na jitahida hizo za watafit, Bwana anawaasa wadau mbalimbali kuzitumia teknolojia hizo ambazo zinawaongezea tija katika kilimo huku wakiwa wanashiriki kutunza mazingira na kuepukana na athari hasi zinazoweza kutokana na mabadiliko ya tabianchi.