TARI yaja na mikakati uzalishaji ngano

SERIKALI kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), imedhamiria kuondoa changamoto ya zao la ngano nchini, inayoipa mzigo mkubwa wa kutumia fedha nyingi za kigeni kuiagiza kutoka nje ya nchi.

Mahitaji ya ngano kwa sasa  kwa mwaka ni tani 1,000,000 na uzalishaji uliopo hapa nchini ni tani 100,000 hivyo kuwa na upungufu wa tani 900,000.

Mratibu wa zao la ngano Kitaifa, kutoka TARI  Kituo cha Selian Arusha, Ismail Ngolida amesema hayo katika maonesho ya wakulima yanayoendelea mkoani Mbeya.

Amesema moja ya mikakati serikali iliyojiwekea ni kuzalisha mbegu za kutosha pamoja na kuongeza maeneo ya uzalishaji wa ngano,  ili ifikapo mwaka 2030 nchi iwe imejitosheleza kwa uzalishaji wa zao hilo.

“Kwa maneno mengine ni kwamba inapofika mwaka 2030 kunahitajika kuwe na uzalishaji unaofikia tani 2500 za mbegu za awali ambazo hizi mbegu za awali zitaweza kuzalisha tani 50,000 za mbegu zilizothibitishwa ubora.

“Mbegu hizi sasa zinaweza kupandwa eneo linalozidi hekta 400,000 ambazo zinaweza kutupatia hayo mahitaji ya ngano,” amesema.

Amesema mwaka huu TARI imeongeza uzalishaji kwa kuwa na zaidi ya tani 250 za mbegu za awali zitakazovunwa kutoka katika mashamba yaliyoko Selian Arusha, Uyole,  Mbeya na Kifyulilo Iringa.

“Lakini vile vile tunataka tuongeze maeneo ya uzalishaji  maana yake ni kwamba tuwe na mbegu ambazo zinaweza kustahimili hata yale maeneo yenye joto lakini  yenye ukame.

“Hivyo tunafanya utafiti wa mbegu mbalimbali na sasa hivi tuna mbegu zinazoweza kustahimili maeneo ya joto la juu lakini vile vile kustahimili ukame, magonjwa ya kutu na sifa nyingine nyingi,” amesema.

Ameyataja maeneo yanayofaa kwa ajili ya uzalishaji wa ngano kuwa ni Tanga, Kigoma, Ruvuma, Geita na Morogoro  hasa eneo la Kilosa.

Maeneo yanayozalisha ngano ni Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Mbeya, Songwe, Rukwa , Njombe na Katavi.

Habari Zifananazo

5 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button