TAASISI ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), imetajirisha wakulima nchini kwa teknolojia mbalimbali ikiwemo utoaji wa elimu, ubunifu na mbinu mbalimbali kwa lengo la kuongeza tija na uzalishaji katika kilimo.
Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dk Geofrey Mkamilo amesema hayo wakati akitoa tathmini ya maonesho ya Nanenane yaliyofanyika kitaifa jijini Mbeya.
Amesema kutokana na teknolojia mbalimbali taasisi hiyo ilizotoa kwa wakulima, imekuwa mshindi wa kwanza katika kanda tano katika kusambaza teknolojia, elimu na utafiti kwa wakulima nchini. Aidha imekuwa mshindi wa pili katika kanda mbili na mshindi wa tatu katika kanda moja.
Dk Mkamilo amesema katika kusimamia hilo la kutafiti, kuhamasisha na kuratibu kilimo kwenye maonesho ya Nanenane katika kanda zote wamepata ushindi baada ya kushindanishwa na taasisi nyingine zinazojihusisha na kilimo nchini.
“Kupitia maonesho mbalimbali yakiwemo ya wakulima, wafugaji na wavuvi TARI imekuwa ikitumia mbinu mbalimbali katika kusambaza teknolojia hilo ndilo limewezesha kupata ushindi huu. Jitihada hizi zinatokana na watafiti wote pamoja na watumishi wa taasisi yetu kwa kuonesha ushirikiano,” amesema.
“Katika ushiriki wake wa kitaifa jijini Mbeya kwenye taasisi za kilimo, TARI ilijinyakulia nafasi ya kwanza katika kuonesha teknolojia mbalimbali za kilimo ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wakulima na wadau wa kilimo.
“Katika viwanja vya Nyakambindi mkoani Simiyu, viwanja vya Nyamhongolo Mwanza, Fatma Mwasa Tabora na Ngongo Lindi vilevile ilishika nafasi ya kwanza kwa kuonesha teknolojia mbalimbali za kilimo, uongezaji thamani wa mazao na utoaji elimu kwa wakulima.
“Katika viwanja vya Nzuguni Dodoma na Themi Arusha, taasisi hiyo ilijinyakulia ushindi wa pili.
“Na katika Uwanja wa JK Nyerere mkoani Morogoro ilijinyakuliwa ushindi wa tatu,” amesema.
Amesisitiza kuwa katika viwanja vyote hivyo TARI imetajirisha wakulima kwa teknolojia mbalimbali za mbegu bora, elimu, zana za kilimo pamoja na upngezaji wa thamani kwa zao husika.
“Ushindi huu umeratibiwa na waratibu mbalimbali wanaofanya tathmini kuhusu wakulima, wafugaji na wavuvi nchini kwa washiriki wote zikiwemo wizara, taasisi mbalimbali za serikali na binafsi, vyuo vya elimu ya juu, halmashauri, taasisi za kimataifa na wadau wa maendeleo,” amesema na kuongeza kuwa kutokana na ushindi huo walipokea kombe na vyeti.