TARURA wafanya kweli barabara Musoma-Bunda

Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo

WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) mkoani Mara inajenga Barabara yenye Kilomita 11, ambayo inaunganisha Wilaya za Musoma na Bunda.

Wakati upande wa Bunda Barabara hiyo inapitia Kijiji cha Karukekere – Mwibara, Musoma Vijijini inapitia Kijiji cha Kinyang’erere kwenye Barabara kuu ya Murangi.

Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo, amesema kijiji hicho ni moja ya vijiji vinne vya Kata ya Bugwema, ambayo sehemu kubwa ni bonde, ambalo serikali imepanga kujenga miundombimu ya kilimo cha umwagiliaji.

Advertisement

“Pamoja na Kinyang’erere, Vijiji vingine ni Bugwema, Masinono na Muhoji,” amesema Prof Muhongo.

Kuhusu barabara inayojengwa amesema ina madaraja mawili kwenye Mito  ya Sijati na Nyamagusu, kwamba itakuwa chachu katika uchumi jimboni kwa sababu ya umuhimu wa Kijiji cha Kinyang’erere, unaotokana na kilimo cha mpunga, dengu, choroko, mahindi, maharage na alizeti.

Kijiji hicho pia imeelezwa kuwa ni mahiri katika ufugaji wa ng’ombe, kondoo na mbuzi.

Mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Kinyang’erere, Sweetbertha Magesa ameshukuru Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Samia Suluhu Hassan kwa kuwaondolea adha walizokuwa wakipata kwa kukosa ya barabara.

“Ilikuwa mtu akitaka kujifungua, anabebwa kwenye mkokoteni utafikiri ni maiti, wengine walikuwa wanajifungulia vichakani kwa kushindwa kutembea mpaka kwenye kituo cha afya,” amesema Magesa.

/* */