TARURA wazungumzia mikakati Barabara Singida

MENEJA WA Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wa Mkoa wa Singida, Mhandisi Tembo David, amesema mpaka sasa wamepokea Sh. Bil. 10.314 sawa na asilimia 48 ya bajeti iliyoidhinishwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara katika Mwaka wa Fedha 2022/2023.

Ameeleza hayo leo, Machi 10 Mwaka huu kwenye kikao cha 46 cha Bodi ya Barabara ya Mkoa huo, chini ya Mwenyekiti wake ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa huo, Peter Serukamba.

“Tulitengewa bajeti ya Sh. 21,436,781,239.08 kwa ajili ya usimamizi, ujenzi na matengenezo ya barabara na mpaka Februari 28 Mwaka huu tulikuwa tumetekeleza mpango wa matengenezo kwa asilimia 66,” amesema Mhandisi David.

Pia bajeti ya Sh.Bilioni 20.159 kwa ajili ya usimamizi na matengenezo ya Km. 893.55 ya barabara za Mkoa huo kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 iliyoandaliwa na TARURA imewasilishwa kwenye kikao hicho.

Amesema asilimia 24 ya mtandao wa barabara za Mkoa huo ndiyo zinazopitika kipindi chote cha mwaka, asilimia 30 zinaridhisha na kwamba asilimia 46 hali yake ni mbaya, zinapitika kwa shida na wakati mwingine mawasiliano hukatika hasa nyakati za masika.

MENEJA wa TANROADS wa Mkoa wa Singida, Mhandisi Msama Msama(Picha zote na Editha Majura).

Naye Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) wa Mkoa wa Singida, Mhandisi Msama K.Msama, pamoja na mambo mengine amesema asilimia 69.6 ya barabara mkoani humo zina hali nzuri, asilimia 24.6, hali yake ni ya wastani na asilimia 5.8 hali yake ni mbaya.

“Hii asilimia ya barabara mbaya inatokana na kuwepo barabara zilizopandishwa daraja kutoka kuwa za wilaya, zikawa za mikoa lakini jitihada zinafanywa kuziweka katika hali nzuri,” amesema Mhandisi Msama.

Maeneo ya hifadhi ya barabara kuvamiwa kwa shughuli tofauti ikiwamo ujenzi na kilimo imetajwa na taasisi hizo kuwa changamoto kwa utekelezaji wa shughuli zao, hali iliyoelezwa kuwa inaendelea kushughulikiwa kwa namna tofauti.

Wakati TANROADS ikishauri wataalamu wa ardhi kushiriki kwenye vikao vya bodi ya barabara ili kuwa na uelewa sawa katika utekelezaji wa majukumu yao, TARURA imesema wametenga fedha kwa ajili ya kuweka mipaka kwenye hifadhi za barabara na imeanza kuweka vibao vya majina ya barabara ili zitambulike.

Habari Zifananazo

Back to top button