Tarura yatakiwa kufikia 85% ya barabara za lami

Ujenzi barabara ya mchepuko mbioni kuanza

WAKALA wa Barabara Vijijini na Mijini wametakiwa kusaka vyanzo vipya vya fedha kwa ajili ya miradi ya barabara za lami mijini na vijijini hadi kufikia 2025.

Akizungumza katika katika kikao kazi na Menejimenti ya Tarura, Makatibu Tawala Wasaidizi Miundombinu, Makandarasi Wazawa, Wataalamu Washauri na Taasisi za Kibenki, kilichofanyika kwenye ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Mohamed Mchengerwa amesema kwa mujibu wa Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi hadi kufikia 2025 Tarura iwe imejenga barabara mijini na vijijini kwa asilimia 85.

Amesema, hatua iliyopigwa mpaka sasa ni ongezeko la barabara kiwango cha lami kutoka 1449.55 hadi 3224.12 sawa na ongezeko la asilimia 122.4 huku barabara za Changarawe zimeongezeka kutoka km 24,405.04 hadi kilometa 41,107.52 sawa na ongezo la asilimia 68.44

Advertisement

“Ilani ya uchaguzi ya CCM imetaka kutekeleza ujenzi wa Barabara nzuri kwa kiwango cha asilimia 85 nchi nzima, tuna kazi kubwa ya kufanya, nimeshazungumza na watendaji wakuu kuona namna gani tufanya kutekeleza maelekezo ya ilani ya uchaguzi,”amesema Mchengerwa na kuongeza

“Ilani inatutaka 2025 tuwe tumejenga barabara kiwango cha tabaka gumu la kupitika mijini, vijijini kote nchi nzima kwa asilimia 85 tunakazi kubwa sana, kwanza kufanya upembuzi katika maeneo yote nchi nzima, kila kijjini, kila halmashauri, kila wilaya, kila kitongoji baada ya hapo tuje na tathmini ya kiwango cha fedha.

Aidha, amesema ameshazungumza na Mtendaji Mkuu Tarura kutafuta fedha ili barabara zote zinazozungumzwa ziweze kujengwa kwa kiwango cha lami, kwa kiwango cha tabaka gumu.

“Ilani ya uchaguzi imelenga kuwaweka pamoja watanzania kimaendeleo, kutatua changamoto za watanzania wa vijiji na mijini barabara ambazo zimekuwa zikiwarahisishia kuingiza bidhaa zao sokoni kupata huduma mbali mbali za kijamii.

“Jukumu ni la kwetu kujiongeza sio kusubiri fedha za serikali ili kupiga hatua, Rais ametoa mwamko kama Tarura, Tamisemi kujiongeza kusaka fedha,”amesisitiza

Awali, Mtendaji Mkuu wa Tarura Mhandisi Victor Seff alisema hadi kufikia Desemba 2023 hatua ya utekelezaji iliyofikiwa ni asilimia 38 ukilinganisha na mpango wa asilimia 40 na jumla ya sh bilioni 241.45 zimepokelewa na Tarura na zimetumika zote.