TASAC kuboresha mtandao wa mawasiliano Ziwa Victoria

TASAC kuboresha mtandao wa mawasiliano Ziwa Victoria

SERIKALI imepanga kuboresha mtandao wa mawasiliano ndani ya ziwa victoria ili kuimarisha usalama wa wavuvi na wasafiri ili kuwawezesha kupata msaada wa haraka pindi wanapokutana na majanga ziwani.

Hayo yalisemwa juzi mjini hapa na Ofisa Mfawidhi wa Shirika la Uwakala wa Huduma za Meli Tanzania (TASAC) Mkoa wa Geita, Rashid Katonga alipokuwa akizungumuza na wavuvi wa mwalo wa Kalilutale wilayani hapa.

Alifafanua kuwa TASAC itaambatanisha mpango huo na ujenzi wa vituo vya utafutaji na uokoaji ndani ya ziwa na utatekelezwa kwa ushirikiano na usimamizi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Advertisement

Alisema hatua hiyo inakuja kutokana na kuwepo kwa changamoto ya mawasiliano katika mwambao wa ziwa Viktoria na maeneo ya jirani ya nchi kavu si tu inawathiri wavuvi bali pia inakwamisha ufanisi wa shughuli za Tasac.

“Shughuli nyingi tunazozifanya Tasac, za usajili, uandaaji wa bili za malipo zinategemea mifumo ambayo inahitaji kuwepo kwa mtandao, kwa hiyo mtandao usipokuwepo huwezi kufanya chochote,” alisema.

Alisema uwepo wa mtandao huo katika ziwa Victoria utaimarisha mawasiliano ya simu na vyombo vya usafiri na kuiwezesha TASAC kutekeleza jukumu la utafutaji na uokoaji kwa urahisi pindi ajali inapotokea.

Alisema mpango umeanza kwanza kwa kung’amua maeneo yenye changamoto, pili kupeleka taarifa kwenye mamlaka husika ambao ni TCRA na kisha kuwapitisha wahusika kwenye maeneo yenye uhitaji.

Awali mmiliki wa vyombo vya uvuvi mwalo wa Kalilutale, Ndange Kiberenge alilalamikia changamoto ya mtandao ndani ya ziwa inahatarisha usalama wa wavuvi hususani inapotokea ajali ama wanapotekwa.

Naye Mvuvi katika Mwalo wa Kalilutale, Zagalo Keberenge mawasiliano yakiboreshwa yatasaidia viongozi waliopo mwaloni kuwasiliana kwa urahisi na wavuvi waliopo ndani ya ziwa wakati wa dharura.

Mkuu wa Idara ya Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Geita, Tito Mlewa aliwahakikishia wavuvi serikali ya awamu ya sita itahakikisha inamaliza changamoto walizonazo ili kuimarisha sekta ya uvuvi nchini.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *