SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) wamebainisha kuwa kwa sasa wameimarisha utendaji kwa kuongeza ukaguzi wa mara kwa mara wa bandari na vyombo vya usafiri ili kudhibiti ajali za majini.
Ofisa Uhusiano Mwandamizi kutoka TASAC, Amina Miruko amesema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya maonesho ya sita ya kimataifa ya teknolojia ya madini mjini Geita.
Amesema ukaguzi huo unalenga kuhakikisha bandari, vyombo vya usafiri na wasafiri vyote vinakuwa salama na kuondoa changamoto inayoweza kujitokeza kutokana na uzembe wa mtu mmoja.
“Tasac pia ina kitengo cha kuratibu utafutaji na uokoaji, kitengo hiki wafanyakazi wake wanafanya kazi masaa 24, ambapo inapotokea dharura yeyote abiria ama mmiliki wa chombo anaweza kupiga simu,”
“Tumefanya kazi kuhakikisha upatikanaji wa ‘life jacket’ unakuwa ni rahisi na upatikanajwa hizo ‘life jacket’ zilizo katika ubora, kwa hiyo tumehakikisha upatikanaji wake unakwa ni rahisi kwa watumiaji wote.
Ofisa usafirishaji kwa njia ya maji kitengo cha kurugenzi ya udhibiti katika bandari kutoka TASAC, Victoria Miyonga amesema wamejiimarisha kusimamia mnyororo mzima wa bandari unakuwa salama.
“Huwa tunafanya kaguzi mbalimbali kwa kuzingatia kwamba waweze kukidhi vigezo, na taratibu ambazo zimewekwa ili huduma wanazozitoa ziweze kuwa bora na watumiaji wapate huduma bila matatizo.”
Victoria amebainisha mpaka sasa kwa Ziwa Victoria Tasac imetoa leseni saba za bandari, leseni mbili za mawakala wa meli, pamoja na leseni tano za wasafirishaji wa mizigo.
Ofisa masoko mwandamizi wa TASAC, Martha Kelvin amesema ajali nyingi za majini zinatokana na uzembe na ukiukaji wa mashariti ya leseni, ambapo mtu anaweza kuwa na leseni ya mizigo lakini anapakia abiria.
Ofisa ugomboaji na uondoshaji shehena kutoka TASAC, Nashon Midagwe amesema katika kuunga mkono sekta madini kwa sasa Tasac wanasimamia uingizaji wa kemikali, mitambo na mashine za uchimbaji.