TASAC yaagiza abiria jeuri washughulikiwe
SHIRIKA la Uwakala wa Huduma za Meli Tanzania (TASAC), limewataka wamiliki na waendeshaji wa vyombo vidogo vya usafiri majini (boti na mitumbwi), kuwaripoti abiria wajeuri wasiotaka kuvaa vifaa vya usalama (Life Jacket).
Ofisa Mwandamizi wa Tasac Mkoa wa Geita, Rashid Katonga ametoa maelekezo hayo wakati akitoa semina ya usalama kwa wadau na watumiaji wa vyombo vya majini wilayani Chato mkoani Geita.
Katonga amesema abiria wa aina hiyo waripotiwe kwa uongozi ama vituo vya polisi kwenye mialo husika, ili waweze kuchukuliwa hatua kwa kuhatarisha usalama wao na kukiuka sheria ya usalama majini.
“Kama mwanzoni amekubali kuvaa ‘life jacket’, anafika katikati ya safari anavua kwa makusudi, tunaamini mwalo ama bandari anayoenda kutua kuna uongozi, kuna vyombo vya ulinzi na usalama.
“Kwa hiyo tunawashauri wanapofika upande wa pili huyo abiria wamripoti kwenye vyombo vya ulinzi na usalama, ili aweze kuchukuliwa hatua na iweze kuwa fundisho,” amesisitiza Katonga.
Amewataka abiria kuzingatia usalama wao, kwani sheria inaelekeza mmiliki wa chombo asipewe leseni hadi awe amekidhi vigezo vya usalama ikiwemo kuwa na idadi ya kutosha ya life jacket kwa wasafiri.
“Endapo huyu mmiliki atakuwa hana life Jacket, zipo kanuni na tarartibu zimeelekeza ambapo ataadhibiwa kwa mjibu wa sheria hizo,” amesema.
Awali Mwenyekiti wa Umoja wa Wamiliki wa Boti Mkoa wa Geita na Kagera, Chaina Kateinawabo ameeleza ipo changamoto kubwa ya abiria wa boti kuonesha ujeuri wanapotakiwa kufuata kanuni za usalama.
Mkuu wa Wilaya ya Chato, Josephati Katwale amewataka Tasac kuendelea kusimamia taratibu, kanuni na sheria za usalama majini pasipo kuangalia mtu ili kuendelea kuepuka ajali za majini kujitokeza.
“Elimu hii (ya usalama majini) inatakiwa itolewe kila mahali na kila wakati, ili kuhakikisha kwamba watu wetu wanaoendesha shughuli zao za uchumi ndani ya Ziwa Vikitoria wanaendesha kwa usalama,” amesema.