BODI ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), imefanya ziara katika Bandari ya Bukoba na kuipongeza serikali kwa hatua kubwa ya upanuzi na ukarabati wa miundombinu ya bandari hiyo ambayo haijawahi kukarabatiwa kwa kiwango kikubwa.
Mjumbe wa bodi hiyo ambaye alimwakilisha Mwenyekiti wa Bodi, King Chiragi amesema kuwa lengo la ziara hiyo ni kuangalia utendaji mkubwa katika bandari za Mkoa wa Kagera, pamoja na ukarabati mkubwa unaofanywa na serikali katika bandari hizo, ikiwa ni pamoja na kuangalia changamoto zilizopo, ili kuzifikisha serikalini na kuzifanyia kazi haraka.
Amesema kuwa uboreshaji wa Bandari ya Bukoba na Kemondo utakapokamilika, basi bandari hizo zinaweza kuwa miongoni mwa bandari zenye mvuto kwa wawekezaji wengi, pamoja na kutoa huduma stahiki kwa wananchi ambao wanazunguka Ziwa Victoria na ukanda wa Africa Mashariki.
“Tumefurahishwa na upanuzi wa bandari pamoja na kazi zinazoendelea hapa katika Bandari ya Bukoba, lengo kubwa la bodi yetu ni kuhakikisha kwamba usafiri wa majini unatoa huduma za kiushindani kwa wananchi sawa na vyombo vingine vya usafiri bila wananchi kujutia kutumia usafiri wa majini ,”amesema Chiragi.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi Bandari (TPA) ya Bukoba, Michael Paranjo amesema kuwa upanuzi wa bandari hiyo na ujenzi wa miundombinu unahusisha ujenzi wa gati jipya, ukarabati wa magati yaliyopo, ujenzi wa jengo la abiria, ujenzi wa miundombinu ya umeme na mifumo ya kuvuna maji mvua kwa gharama ya Sh bilioni 19.5
Comments are closed.