Shirika la Uwakala wa Meli nchini (TASAC) limetoa elimu ya ulinzi, na utunzaji wa mazingira kwa wananchi wa wilaya ya Ifakara, Morogoro.
Akizungumza na wananchi waliojitokeza kwenye mafunzo hayo mwishoni mwa juma, Afisa Ukaguzi na Mdhibiti wa vyombo vya majini wa TASAC, Gabriel Manase amesema kuwa zoezi hilo lililolenga kuwajengea uelewa wananchi hao katika maeneo hayo, limeanza Novemba 11, 2022 huko Ifakara na kwamba litaendelea katika mikoa mingine ya Iringa na Dodoma.
“Zoezi hili ni endelevu limeanza hapa Ifaraka Novemba 11, mwaka huu katika maeneo ya, Ngalimila, Ngapemba, Utengule, Chita, Mngeta na Mchombe na linaendelea katika mikoa ya Iringa na Dodoma,” amesema Manase.
Shirika hilo limekuwa na utaratibu wa kutoa elimu juu ya masuala mbalimbali yakiwemo ulinzi, usalama na utunzaji mazingira kwa wananchi wanaotumia vyombo vya majini pamoja na wale wanaofanya shughuli zao za kiuchumi majini kwa kuhakikisha wanapata uelewa wa kutosha ili elimu hiyo iwasaidie wanapokuwa kwenye majukumu yao ya kila siku wanapotumia vyombo vya usafiri majini.
Mbali na majukumu hayo, TASAC wameendesha zoezi la ukaguzi wa vyombo vya usafiri majini vinavyotumika katika eneo hilo.
Hata hivyo, huo ni mwendelezo kwa TASAC kukutana na wananchi katika maeneo mbalimbali na kuwapa elimu kwa kuhakikisha kunakuwepo na ulinzi, usalama na utunzaji mazingira katika maeneo yote ya bahari, maziwa, mito na mabwawa.