Tasac yatoa mwelekeo tozo mpya za TPA

SHIRIKA la Uwakala wa Meli nchini (TASAC) limesema litazingatia maoni yaliyotolewa na wadau wa usafirishaji  majini mkoani Kigoma kuhusiana na maombi ya mamlaka ya usimamizi wa bandari nchini (TPA) kupitia na kupanga upya tozo mbalimbali katika bandari zake nchini na kwamba tozo zitakazopitishwa zitazingatia uhalisia wa utoaji huduma kwa pande zote.

Mkurugenzi wa udhibiti wa usafiri kwa njia ya maji kutoka TASAC,  Deogratius Mukasa alisema hayo akihitimisha mkutano wa siku moja wa wadau hao uliojumuisha watoa huduma mbalimbali katika bandari za Ziwa Tanganyika wakitoa maoni na mapendekezo ya marekebisho ya tozo zilizowasilishwa na uongozi wa TPA.

Mkurugenzi huyo wa udhibiti ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TASAC alisema kuwa ukusanyaji huo wa maoni utaendelea hadi Julai 20 mwaka huu na baada ya hapo maoni ya wadau wa bandari yaliyokusanywa kulingana na mapendekezo ya TPA yaliyowasilishwa kwa wadaub yatapelekwa kwenye vikao vya bodi  za TASAC ili kuweka uwiano wa viwango vinavyokusudiwa kulingana na hali halisi ya huduma inayolengwa.

Advertisement

Hata hivyo alisema kuwa kikao hicho kimeonyesha kutimiza malengo yake kutokana na walengwa kukubaliana na baadhi ya mapendekezo yaliyowasilishwa na TPA lakini pia wakitaka baadhi ya tozo kupunguzwa na nyingine kuondolewa kutokana na kuwa mzigo kwa wadau, wasafirishaji shehena na wananchi.

Baadhi ya wadau waliohudhuria mkutano huo wa kukusanya maoni kulingana na mapendekezo ya marekebisho ya tozo yanayokusudiwa kufanya na Mamlaka ya usimamizi wa bandari nchini (TPA) walisema kuwa bado maboresho makubwa yanapaswa kufanywa kwenye viwango hivyo vya tozo.

Mmoja wa wadau hao Brian William, wakala wa forodha katika mwambao wa Ziwa Tanganyika alisema kuwa kwenye mapendekezo yao wameomba kuboreshwa kwa tozo kupunguzwa viwango vyake kwake bado zimekuwa mzigo kwa wasafirishaji wa shehena na wadau wanaotumia bandari za ziwa Tanganyika kupitia Bandari ya Dar es salaam wakieleza kuwa tozo hizo bado ni kubwa na zinakimbiza wateja.

Naye Dunia Shakuru Wakala wa meli kutoka kampuni ya DS SALUTA & SONs Ltd alisema kuwa zipo tozo ambazo hazipaswi kuwepo na zinapaswa kuondolewa kabisa ikiwemo tozo ya shilingi 600 wanayotozwa wananchi wanaosafiri na vyombo mbalimbali kwenye ziwa Tanganyika wakati wanasafiri ndani ya nchi na tozo hiyo haina maana yeyote.

1 comments

Comments are closed.