TASAF yapewa wiki mbili kulipa malimbikizo ya walengwa

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene ameupa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (TASAF) hadi Machi 5, mwaka huu uwe umelipa malimbikizo yote yanayodaiwa na walengwa wa mpango huo nchini kote.

“Uongozi wa pamoja umesaidia sana utekelezaji mzuri wa miradi hii ya TASAF. Lakini kuna kelele kubwa katika mradi huu, kelele hiyo ni ile inayohusu ucheleweshaji wamalipo kwa walengwa; Nasema tusimgombanishe Mheshimiwa Rais na walengwa. Ni haki yao kulipwa fedha zao kwa wakati na hiyo ndiyo njia itakayoondoa kelele hizo,” alisema.

Simbachawene ameyasema hayo katika ziara yake ya kutembelea wanufaika wa mradi huo unaolenga kupunguza umaskini na kuboresha maisha ya watu waishio katika mazingira magumu aliyoifanya Iringa Vijijini katika vijiji vya Migori na Kinywang’anga jimboni Isimani.

Wakati katika kijiji cha Kinywang’anga kuna kaya 34 zilizotambuliwa na kuingizwa katika mpango huo unaohusu uhawilishaji (ugawaji) fedha kwa walengwa, ajira za muda na uwekaji akiba kupitia vikundi, katika kijiji cha Migori kuna kaya 117 zinazonufaika.

“Kwa kuwa kila kitu kipo sawa, lazima tuwasimamie mtoe malipo hayo kwa wakati. Mkifanya hivyo zaidi ya muda huu ambao tumekubaliana, serikali haiwezi kukubali na hatuwezi kumuacha mtu salama,” alisema bila kutaja kiwango kinachodaiwa.

Simbachawene alisema mpango wa TASAF ni wa kupigiwa mfano kwa kuwa unalenga kuongeza kipato cha kaya na kuwekeza katika afya na elimu ya watoto, kuinua uchumi kwa kujenga uwezo kwa kaya katika utunzaji rasilimali na kutengeneza njia mbadala na endelevu za ajira na kushiriki katika kazi za jamii na kupata kipato cha ziada kwa matumizi ya chakula na kugharamia mahitaji mengine ya msingi huku wakiboresha miundombinu katika jamii na kupata ujuzi na stadi za maisha.

Alisema kaya masikini zilizokosa fursa ya kusajiliwa katika awamu zilizopita zisubiri awamu inayojuka itakayohusisha pia kuziondoa katika mpango huo kaya ambazo maisha yake kwa kupitia utekelezaji wa shughuli za mpango maisha yao yamebadilika kwa kuwa nafuu na bora kuliko ilivyokuwa awali.

“Kipindi cha Pili cha TASAF Awamu ya Tatu kililenga kuongeza kipato na kuboresha huduma za kiuchumi na kijamii kwa walengwa na kulinda maslai ya watoto wao. Tunaamini wapo wengi ambao mambo yao yamebadilika katika kipindi hicho ambao wanapaswa kutoka katika mpango ili kuruhusu wengine wenye maisha duni kuingia,” alisema.

Aliiagiza TASAF katika awamu ijayo ya mpango huo kuwekaza nguvu zaidi katika kusajili kaya masikini zenye watu wenye ulemavu ili kuendelea kumpa faraja Rais Dk Samia Suluhu Hassan anayetaka kuona mpango huo unagusa makundi mengi zaidi yenye uhitaji.

Wakati huo huo, Simbachawene amesema serikali inafikiria kubadili jina la mpango huo kutoka “Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini” na kuwa “Mpango wa Kuboresha Maisha ya Wananchi.”

“TASAF ni uwekezaji mkubwa sana, ni mfano bora katika kuondoa umasikini, inashirikisha wananchi na ni uwezeshaji wa wananchi kiuchumi-ina miradi ya mfano na ya gharama nafuu inayogusa maisha ya mwananchi huku huduma zake zikiunganisha masikini na matajiri ili wazipate kwa pamoja, kwahiyo huko mbele ni muhimu tukabadili jina lake,” alisema.

Awali Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Iringa, Venance Ntiyalundura alisema tangu kuanzishwa kwake, mpango huo umewezesha mkoa wa Iringa wenye zaidi ya walengwa 30,000 kupata zaidi ya Sh bilioni 16.8 ambazo kati yake zaidi ya Sh bilioni 13 zimegaiwa kama ruzuku kwa wanufaika hao huku zinazobaki zikienda kwenye miradi inayotoa ajira za muda na kwa ajili ya vikundi vya kukopa na kurejesha.

Katika kijiji cha Kinywang’anga, Simbachawene alitembelea mradi wa birika la kunyweshea mifugo katika kijiji cha Migori alitembelea shamba la parachichi, yote ikiwa imefanywa na walengwa wa mpango huo katika vijiji hivyo.

Habari Zifananazo

Back to top button