TASWA, IPRT wakubaliana kunoa wachambuzi, wasemaji

CHAMA cha Waandishi wa Michezo Tanzania (TASWA) na Taasisi ya Uhusiano wa Umma Tanzania (IPRT), wamesaini makubaliano ya ushirikiano wa kimkakati wenye lengo la kukuza na kuendeleza waandishi wa habari za michezo na tasnia ya michezo kwa ujumla.

Tukio la kusaini Mkataba wa Ushirikiano(MoU) limefanyika leo jijini Dar es Salaam, likihusisha viongozi waandamizi wa taasisi hizo mbili akiwemo Mwenyekiti wa TASWA Amir Mhando, Katibu Mkuu wa chama hicho Alfred Lucas na Mkurugenzi wa IPRT William Kallaghe.

Akizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo Kallaghe amesema wamehitimisha mazungumzo ya muda mrefu na uongozi wa chama hicho kuona namna ya kuwepo mafunzo ya kitaaluma na ya sekta ya michezo kwa waandishi wa habari za michezo na wachambuzi wa habari za michezo kwa ujumla hapa nchini.

“Kutakuwa na programu ya mafunzo maalum ya mawasiliano na uongozi, ambayo imeandaliwa kwa ajili ya watendaji wakuu na itajikita katika kuendeleza ufahamu sahihi wa maadili na ujuzi wa ngazi ya  chini na juu  ili kufikia malengo ya mafanikio kitaasisi.

“Pia kutakuwa na mafunzo ya wazi ya mawasiliano na uongozi, eneo hili ni maalum kwa ajili ya wahariri wa habari za michezo, wasemaji wa klabu na vyama vya michezo, watendaji na mameneja wa ngazi ya kati.

“Mafunzo kwa waandishi wa habari za michezo na wachambuzi, hii ni programu ya mafunzo maalum inayolenga kuwajengea uwezo waandishi wa habari za michezo, waandishi waandamizi wa habari za michezo na wachambuzi wa habari za michezo,”  amesema Kallaghe.

‘’Ushirikiano huu unawakilisha hatua muhimu katika kutumia nguvu za mawasiliano yenye ufanisi wa hali ya juu na uongozi thabiti katika kufanikisha ukuaji na maendeleo ya michezo nchini.

“ Tunaamini kwamba kwa kufanya kazi pamoja na TASWA, tunaweza kufikia matokeo ya mazuri zaidi na yenye tija kubwa katika maendeleo ya kimichezo na kiuchumi ya nchi yetu,” amesema Kallaghe.

Lucas amesema eneo lingine ambalo limetiliwa mkazo ni mafunzo ya uwezeshaji wa wanawake waandishi wa habari za michezo ili kuwajengea uwezo zaidi na kuongeza kuwa wamefurahi kuingia ushirikiano huo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TASWA, Amir Mhando amewaomba wanahabari kushirikiana katika jambo hilo mara baada ya utaratibu huo wa mafunzo kuanza na kusisitiza kuwa ni dhamira ya chama chao kuwafikia wote katika maeneo mbalimbali nchini.

 

Habari Zifananazo

Back to top button