MWAKILISHI wa Kudumu wa Tanzania katika Ofi si za Umoja wa Mataifa (UN) jijini New York nchini Marekani, Balozi Profesa Kennedy Gaston amesema taswira ya Tanzania kimataifa ni nzuri.
Amesema jumuiya ya kimataifa inaiona Tanzania ni nchi yenye amani na utulivu na kinara wa kupambana na changamoto mbalimbali zikiwamo za ugaidi na nyingine za uhalifu wa kikanda.
Balozi Profesa Gaston alisema hayo jana akiwa New York wakati akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano uliofanywa kwa njia ya video kuhusu mrejesho wa Mkutano Mkuu wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA77) uliomalizika hivi karibuni.
Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alihudhuria mkutano huo akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan. Balozi Profesa Gaston alisema Tanzania katika mkutano huo iliwakilishwa vyema na Dk Mpango ambaye alipata nafasi mara kadhaa kuhutubia mkutano huo na mingine na kuungwa mkono na jumuiya ya kimataifa.
“Changamoto za ndani ya nchi kama hayo masuala ya ‘panya road’ ni mambo ambayo nchi inayashughulikia ndani. Tanzania inaonekana kinara wa kupambana na changamoto kama ya ugaidi na nyingine za uhalifu wa kikanda,” alisema Balozi Profesa Gaston.
Aliongeza: “Imekuwa nchi ya mfano kwa amani na kuleta maendeleo, matatizo ya ndani hayajachafua taswira ya Tanzania hata kidogo, bado ni kisiwa cha amani, tulivu na ni mfano wa kuigwa kwa mataifa mengine yanayoendelea, hii ndio taswira ya Tanzania kimataifa.” Alisema katika mkutano huo, zaidi ya nchi 193 zilikuwa na mtazamo chanya na uongozi wa Rais Samia na dhana ya demokrasia inavyochukuliwa nchini na zimeifanya nchi kuwa mfano tafsiri ya nchi zinazoendelea.
“Rais Samia amezidi kuiweka Tanzania kwenye taswira ya nchi inayoleta ushirikiano na maendeleo endelevu kwa ustawi wa jamii,” alieleza Balozi Profesa Gaston.
Alibainisha kuwa Tanzania ndani ya UN imekuwa mwanachama na mshiriki mzuri katika misheni mbalimbali, na ni nchi ya 13 kati ya nchi za UN zinazotoa askari wa ulinzi wa amani na inashiriki katika misheni tano kati ya 15 za umoja huo.
Alisema mbali ya mkutano huo wa UNGA77, Tanzania pia ilishiriki mkutano mwingine pembeni ya huo wa kuchangia Mfuko wa Kupambana na Malaria. Dk Mpango alihutubia na kueleza namna Mfuko wa Global Fund ulivyo mstari wa mbele kusaidia Tanzania na kusema tangu uanze kufanya kazi nchini mwaka 2003 hadi sasa umeshaipa nchi Dola za Marekani bilioni 2.8.
“Katika hilo, pia Dk Mpango alieleza mchango wa Tanzania ndani ya mfuko huo kuwa imeshatoa Dola za Marekani milioni moja, hii ilifurahiwa sana na wakuu wa nchi washiriki na Umoja wa Mataifa kuona Tanzania inavyoshiriki,” alisema.
Aidha, alisema Dk Mpango pia alishiriki mkutano wa kilele wa mageuzi ya elimu uliofanyika Septemba 19, mwaka huu ukiwa na madhumuni ya kuweka elimu kwenye ajenda ndani ya Umoja wa Mataifa. Alisema nchi mbalimbali zilitoa ahadi za kuboresha elimu na Tanzania ilitoa tamko ambako UN ilitangaza chombo cha kimataifa cha ufadhili elimu na kuzinduliwa kwa programu ya mafunzo kwa njia ya kidijiti.
Aidha, alisema Tanzania iliahidi kuongeza bajeti ya elimu kutoka asilimia 18 ya bajeti ya sasa hadi 20. Pia akizungumzia yaliyojiri katika mkutano wa malengo endelevu, ambao nchi wanachama zilielezwa umuhimu wa kuleta maendeleo na kupambana na changamoto ya ukosefu wa chakula, kupanda kwa bei ya mafuta na athari za janga la virusi vya corona.
Katika mkutano wa kutokomeza matumizi ya silaha za nyuklia, Tanzania ilisisitiza umuhimu wa kuondoshwa kwa matumizi ya silaha hizo na iliunga mkono juhudi kuhusu hilo, na kwamba Bunge la Tanzania linaendelea na mchakato ili kuridhia mkataba wa kuondoa matumizi ya silaha hizo kwa sababu madhara yake ni makubwa.