MOROGORO:Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), imesema itaendelea kuimarisha ulinzi wa wananchi na mali zao dhidi ya wanyamapori wakali na waharibifu.
Kamanda wa Kanda Maalumu ya Uhifadhi Dar es Salaam wa Mamlaka hiyo , Kamishna Msaidizi Mwandamizi , Sylvester Mushi amesema hayo wakati akimkaribisha Mkuu wa wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro, Judith Nguli.
Mkuu huyo wa wilaya alikuwa mgeni rasmi wa kuzindua vikundi 12 vya kujitolea vya kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu , na ugawaji vifaa vilivyotolewa Mamlaka hiyo.
Hafla hiyo imefanyika kwenye Kata ya Melela, Tarafa ya Mlali wilayani humo ambapo vikundi hivyo vya kujitolea kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu vimeundwa kutoka vijiji 11 vilivyopo katika kata nne za Wilaya Mvomero zenye changamoto kubwa ya Wanyamapori wakali na Waharibifu.
Kata hizo zipo kwenye eneo linalosimamiwa na Mamlaka hiyo ambazo ni Melela, Lubungo, Mlali na Dakawa (Wami Dakawa), ambapo vikundi hivyo vilivyopatiwa mafunzo vimegawiwa vifaa ambavyo ni tochi za mwanga mkali 120, vuvuzela 120 na filimbi, 120 thunder flash 600 na roman candle 600 na vitakuwa na uwezo wa kudhibiti wanyamapori watakaovamia mashamba na mazao kwa haraka kabla askari wahifadhi kufika.
Kamanda wa Kanda Maalumu ya Uhifadhi inajumuisha mkoa wa Pwani, Dar es Salaam na Morogoro amesema hatua hiyo ni kupunguza madhara yanayosababishwa wanyamapori hususani tembo kwenye uharibifu wa mazao ya wananchi.