TAWOMA waanzisha tuzo malkia wa madini

CHAMA Cha Wachimbaji Wadogo Wanawake Nchini (TAWOMA) kimeanzisha na tuzo za Malkia wa Madini ikiwa ni sehemu ya kutambua na kuhamasisha juhudi za uwekezaji wa wanawake katika sekta ya madini.

Mwenyekiti wa Tawoma Taifa, amebainisha hayo katika hafla ya kwanza ya kitaifa ya utoaji tuzo hizo iliyofanyika juzi mjini Geita na kueleza wamedhamiria kuzalisha mabilionea wanawake kupitia madini.

Amesema ikiwa Tawoma imetimiza miaka 25 wameamua kuwafanya wanawake kuwa vinara na wawekezaji wakubwa kwenye sekta ya madini badala ya kubakia kuwa wasindikizaji na vibarua.

“Tumekuja na malkia wa madini tuweze kumtafuta mwanamke anayelipa kodi zaidi, mwanamke anayesimamia usalama, mwanamke anatunza mazingira na mwanamke anayetoa ajira nyingi.”

Semeni ametaja kikundi cha mshikamano kutoka Kahama Shinyanga kuwa wanawake wa mfano ambao ndani ya mwaka mmoja wameiingizia serikali takribani Sh bilioni 3 ikiwa ni malipo ya maduhuli.

Amebainisha mpaka sasa kuna mwamko mkubwa kwa wanawake katika ekta ya madini ambapo mpaka sasa kuna wanachama 4,000 kutoka mikoa 21 na wilaya 46 pamoja na vikundi 1,500 vilivyosajiliwa.

Amesema Tawoma imebeba jukumu la kuwawezesha wanawake wachimbaji kwa kuwajengea uwezo waweze kupita hatua kwenze matumizi za teknolojia sahihi katika uchimbaji na uchenjuaji wa madini.

Mwenyekiti wa Tawoma mkoa wa Morogoro, Merry Kombe amesema sera rafiki za madini zimehamasisha wanawake kuingia kwenye biashara ya madini ambayo awali ilionekana kuwa kazi za wanaume.

Mshindi wa Tuzo ya Malkia wa Madini 2023, Alice Kyanila amekiri tuzo hiyo ni kampeni sahihi kuwainua wanawake kuwa washindani kwenye sekta za madini na kuchangia mapato makubwa serikalini.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amewahakikishia Tawoma serikali itaendelea kuwaunga mkono kwa kuwawezesha kufanikisha uwekezaji wao kuanzia kwenze uchimbaji, uchenjuaji hadi sokoni.

“Mnafanya kazi nzuri sana, naamini kupitia umoja huu siku moja tutazalisha mabilionea wengi sana akina mama kwenze sekta hii za madini.”

Habari Zifananazo

Back to top button