Tax: Samia amewapigania sana waliokuwa Sudan

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax amesema huruma ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa raia wake imewezesha kuwarudisha nyumbani Watanzania kuepuka madhara ya machafuko nchini Sudan.

Aidha, Dk Tax ameagiza raia wote wa Tanzania wanaoishi na kufanya kazi nje ya nchi wajisajili ili watambulike katika balozi za Tanzania.

Aliyasema hayo jana wakati alipowapokea Watanzania 206 kutoka Sudan kwa ndege ya Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) ya Boeing 787-8 Dreamliner iliyotua saa 3:15 asubuhi wakitoka Addis Ababa nchini Ethiopia.

Alisema Rais Samia aliamua kuhakikisha hakuna Mtanzania atakayedhurika kutokana na mapigano nchini humo hivyo alitoa ndege na kugharamia safari za raia hao kutoka sehemu mbalimbali hadi nchini Ethiopia na baadaye kusafirishwa hadi Dar es Salaam.

“Amewapigania sio mchezo. Zoezi hili halikuwa rahisi hata kidogo, tulianza kusafiri kwa mabasi kutoka Khartoum hadi mpakani mwa Ethiopia panaitwa Matema kilometa 900,” alisema Dk Tax.

Alisema katika Mji wa Matema kulikuwa na taratibu za kawaida za kiuhamiaji, lakini walipita bila tatizo kutokana na ombi la Rais Samia kwa Serikali ya Ethiopia.

Alisema kutoka Matema Watanzania hao walisafiri hadi katika Mji wa Gota ambao una kiwanja cha ndege ambacho kingeweza kutumika kuwasafirisha moja kwa moja hadi Dar es Salaam, lakini kilikuwa ni kidogo ikilinganishwa na ndege ya Dreamliner.

“Ilibidi tukodi ndege nyingine pale ambayo ilitumika kuwachukua raia wetu kutoka pale hadi mjini Addis Ababa iliyolazimika kufanya safari mbili kwa kuwa ilikuwa ndogo ambapo alfajiri ya leo (jana) walifika Addis Ababa na kuikuta ndege yetu ikiwa tayari,” alibainisha Dk Tax.

Miongoni mwa Watanzania waliowasili jana, wanafunzi ni 150, diaspora 22, maofisa wa ubalozi 28 na wafanyabiashara sita.

Balozi wa Tanzania nchini Sudan, Silima Kombo Haji alisema kazi ya kuwakusanya raia wa Tanzania ili kuwasafirisha ilikuwa ngumu.

Balozi Haji alisema taarifa zilizopo katika ofisi yake kuna Watanzania watatu ambao ni wafanyabiashara ambao walitaka kuja, lakini walishindwa kutokana na matatizo ya pasipoti na walielekezwa wakae katika maeneo ya ubalozi ili kuendelea kuwa salama.

Mwakilishi wa wazazi wa watoto wanaosoma nchini Sudan, Rashid Kilindo alimshukuru Rais Samia kwa kuwezesha kuokolewa kwa watoto wanaosoma katika vyuo mbalimbali nchini humo.

Kiongozi na mwakilishi wa wanafunzi wanaosoma nchini Sudan, Salmini Banga alimshukuru Rais Samia na Watanzania wote kwa ujumla kwa dua zao na jitihada za kuhakikisha kuwa wanarudi nchini salama.

Habari Zifananazo

Back to top button