TBA yajipanga kuwafikia wachimbaji wadogo geita

GEITA:WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) wamepanga kujenga nyumba za kupangisha mjini Geita ili kusaidia watumishi wa umma na wananchi wa kawaida ikiwemo wachimbaji wadogo kupata makazi bora.

Meneja wa TBA Mkoa wa Geita, Mhandisi Gladys Jefta amesema hayo mbele ya waandishi wa habari katika maonyesho ya sita ya kimataifa ya teknolojia ya madini yanayoendelea mjini Geita.

Amesema huo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ambapo akizindua nyumba za watumishi eneo la Magomeni Mapipa aliagiza TBA kuanza kujenga nyumba za kupangisha wananchi wa kawaida.

“Alitupa maelekezo kwamba TBA sasa tujitanue, tusiwe tu kwenye kujenga nyumba za watumishi wa umma lakini tuungane na wawekezaji kujenga nyumba za watumishi lakini pia nyumba za watu wengine.

Ameongeza pia mabadiiko ya kisheria yanawaunga mkono kwani GN 595 ya Agosti 23, 2023 imewaelekeza TBA kujitanua zaidi kwa kushirikiana sekta binafsi na kutokujikita kwenye sekta za umma pekee.

Amefafanua eneo la mradi ni mtaa wa Mission kata ya Kalangalala na utekelezaji utaanza kwa mwaka huu wa fedha mara baada ya ubunifu na tathimini kukamilika kwa ajili ya kupata gharama halisi za mradi.

Gladys ametaja baadhi ya miradi waliyoitekeleza mkoani Geita ni ofisi ya Halmashauri mbogwe, hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Geita, hospitali ya rufaa ya kanda Chato pamoja na ofisi za Tanesco Geita na Chato.

Habari Zifananazo

Back to top button