WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA), imekamilisha na kukabidhi mradi wa majengo ya Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) ofisi za Mkoa wa Geita na Wilaya ya Chato zilizogharimu takribani Sh bilioni nane.
Akizungumza katika makabidhiano hayo, Kaimu Meneja wa TBA Mkoa wa Geita, Ofisa Mkadiriaji Ujenzi, Glory Akyoo, amesema miradi hiyo imekamilika kwa asilimia 100 na ipo tayari kwa matumizi.
Amefafanua majengo ya ofisi ya Tanesco Mkoa wa Geita na ofisi ya Tanesco Chato yamegharimu kiasi cha Sh bilioni nne kila moja na miradi hiyo ni imetekelezwa kuanzia ubunifu mpaka ujenzi.
Amesema miradi hiyo ni sehemu ya miradi minne ya buni jenga iliyotekelezwa na TBA mkoani Geita mingine, ikiwa ni majengo ya hospitali ya rufaa ya kanda Chato na hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Geita.
“Utekelezaji wa mradi umeenda vizuri, na leo Janauri 11,2023 tumefanikiwa kukabidhi kwa wahusika, ili aweze kuendelea na mradi,” Amesema na kuongeza;
“Tunaishukuru serikali na tunaipongeza, na tunaiomba iendelee kutuamini katika kutekeleza miradi. Majengo yote yamezingatia ubora na tumekuwa tukitekeleza miradi hii kwa kuzingatia viwango.”
Meneja Usanifu na Ubunifu TBA makao Makuu, Godfrey Mwakabole amesema mradi umetekelezwa kwa kuzingatia gharama, muda na vigenzo kadri ya mkataba kuanzia mwanzo hadi kukamilisha.
Mhandisi Msimamizi wa Mradi, Devotha Kaboko amesema mradi huo ulianza kutekeleza Desemba 2, 2019 na umekamilika Desemba 31, 2022 na majengo yote yamefuata vigezo vya majengo ya serikali.
Meneja wa Tanesco Mkoa wa Geita, Mhandisi Grace Ntungi amesema ukaguzi umefanyika na majengo yamekidhi vigezo vya watoa huduma na wateja na kuondoa kero ya kukodi majengo kwa miaka tisa sasa.
“Jengo hili jipya litasaidia wateja wetu kututembelea na kupata huduma katika mzingira mazuri na pia itatusaidia kwa wafanyakazi kuongeza ari na kufanya kazi kwa bidii kwa sababu mazingira ni rafiki,” amesema.