TBA yasisitiza mambo mazuri zaidi yanakuja

WAKALA wa Majengo nchini (TBA), imewahahakikishia Watanzania kuwa itaendelea kubuni, kutathmini, kutekeleza na kusimamia miradi ya ujenzi kwa ufanisi, kwani serikali imeweka mazingira wezeshi kwa TBA kuwajibika.

Meneja Uhusiano kwa Umma wa TBA, Fredrick Kalinga,  amesema hayo kwa waandishi wa habari katika maonesho ya tano ya teknolojia ya madini yanayoendelea kwenye viwanja vya Bombambili mjini Geita.

Amesema tayari serikali imeshafanyia kazi changamoto zilizokuwepo TBA, ikiwemo uhaba wa watumishi, vitendea kazi na hivyo wana uhakika miradi yote wanayosimamia inakamilika kwa wakati.

“Pale katika mji wa serikali Mtumba Dodoma tumefanya mradi wa majengo ya serikali na wizara 28, ambapo moja ya jengo hilo ni ofisi za wizara ya madini, ambapo kwa sasa tunafanya usimamizi na mradi huo umefikia asilimia 58.

“Tuna majengo matatu ambayo tumeyajenga katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Geita, lakini tuna majengo matano ambayo tumeyajenga katika hospitali ya rufaa ya kanda Chato na majengo sita ya ofisi mbalimbali hapa mkoani Geita.

“Vile vile tuna mradi mkubwa wa nyumba za watumishi 3,500 pale Nzuguni Dodoma, ambapo hapa tumekuwa tukiwaonesha wananchi pamoja na watumishi ambao wanafanya kazi na wamekuwa na shauku ya kuona mradi huo,” amesema.

Akizindua maonesho hayo, Waziri wa Madini, Dk Dotto Biteko ameipongeza TBA na kuitaka kuongeza ufanisi katika kukamilisha miradi kwa wakati.

Habari Zifananazo

Back to top button