TBA yatumia kadi kubana wapangaji

WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) umeweka mfumo wa kidijiti kwenye kitasa janja usioruhusu mpangaji kuingia ndani kama anadaiwa. Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa ameipongeza TBA kwa kuweka mfumo huo wa kutumia kadi ambayo imeshalipiwa ili kuingia ndani ya nyumba.

Profesa Mbarawa alitoa pongezi hizo jijini Arusha baada ya kukagua maendeleo ya jengo la kitega uchumi la ghorofa 10 lenye uwezo wa kuchukua familia 22. Alisema jengo hilo litapunguza changamoto za makazi kwa watumishi wanaofanya kazi katika ofisi za serikali mkoani humo. “Mfumo huu ni mzuri sababu ambaye hajalipa hatakuwa na uwezo wa kuingia ndani kwake lakini utawapunguzia sana usumbufu, hongereni sana,” alisema Profesa Mbarawa.

“Niwapongeze TBA kwa kuja na mradi huu na nimeridhishwa na hatua iliyofikiwa kwani jengo hili linaendana na thamani ya fedha ambazo zimetumika hapa na ni matumaini yangu mapato yataongezeka na kuongeza majengo mengine kama haya katika miji,” alisema Profesa Mbarawa.

Kaimu Meneja wa TBA Mkoa wa Arusha, Juma Dadi alimweleza Profesa Mbarawa kuwa hadi sasa wamepokea maombi takribani 40 ya wapangaji katika nyumba hizo hali inayowapa motisha ya uhitaji zaidi wa nyumba katika mkoa huo.

Dandi alisema kukamilika kwa jengo hilo kutaongeza pato la TBA na serikali kwa kwa kuwa idadi ya nyumba wanazozimiliki imeongezeka na wametenga fedha ili kujenga nyumba nyingine za biashara kama hizo.

Alisema mradi huo umeongeza idadi ya ajira kwa mafundi na wafanyakazi wengine na kuwepo kwa ununuzi wa vifaa vya ujenzi.

Jengo la Kitega Uchumi la Makazi mkoani Arusha limegharimu Sh bilioni 5.5 na kwa sasa limefikia asilimia 98 na linatarajiwa kukamilika mwezi ujao.

Habari Zifananazo

Back to top button