TBS: Zingatieni ubora
MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt Athuman Ngenya amewaasa wazalisha bidhaa kuzingatia suala la ubora unaokidhi viwango vya taasisi hiyo kwenye bidhaa wanazoenda kuzalisha.
Ngenya, amebainisha hayo mapema leo jijini Dar es Salaam kwenye hafla ya kukabidhi vyeti na leseni za ubora kwa wazalishaji wa bidhaa kutoka mikoa iliyopo kanda ya Mashariki.
“Niwapongeze wazalishaji wote na napenda kuwaasa kuwa muwe mabalozi wazuri wa TBS kwa kuhakikisha bidhaa mnazozizalisha zinakuwa na ubora,” amesema Ngeya.
Awali, Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora (TBS), Lazaro Msasalaga alisema serikali imetenga fedha kupitia TBS kwa lengo la kuwapatia wazalisha bidhaa leseni ya kutumia alama ya ubora bila gharama yoyote.
Katika hafla hiyo TBS imetoa vyeti na leseni 264 kwa wazalishaji wa bidhaa mbalimbali, katika leseni hizo leseni 107 ni kwa wajasiriamali wadogo waliothibitishwa taasisi hiyo.