TCAA yatamani makubwa kimataifa
DAR ES SALAAM; MAMLAKA ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), imebainisha kuwa imejizatiti kuboresha huduma za usafiri wa anga nchini na kufikia viwango vya kimataifa, ili kuwezesha mashirika mengi ya kimataifa kutumia anga la Tanzania na hivyo kuchagiza ukuaji wa sekta mbalimbali.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari wakati akipokea mitambo ya mawasiliano ya sauti kati ya rubani na waongozaji ndege.
Pia amesema amesema mamlaka imewapeleka wataalamu 24 kwenda nchini Italia na Norway, ili kupata mafunzo ya uendeshaji wa mitambo hiyo itakayofungwa katika Uwanja vya Julius Nyerere, Dar es Salaam, Pemba, Songwe, Abeid Karume Zanzibar, Mwanza, Tabora, Kigoma, Dodoma, Mtwara, Tanga, Kilimanjaro na Arusha.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa huduma za uongozaji ndege kutoka mamlaka hiyo, Flora Mwanshinga amesema kwa sasa sekta hiyo imekuwa ikipitia changamoto mbalimbali za mawasiliano kutokana na mabadiliko ya teknolojia, hivyo kuja kwa mitambo hiyo kutasaidia kuongeza ufanisi wa huduma.