BARAZA la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano Tanzania (TCRA CCC) imeishukuru serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuondoa tozo ya miamala ya simu.
Katibu Mtendaji wa TCRA CCC, Mary Shao Msuya akizungumza na HabariLeo leo Julai 12, 2023 amesema kuondolewa kwa wa tozo hizo kunaendelea kuchochea ukuaji wa matumizi ya fedha kidigitali na kuimarisha usalama wa fedha za watumiaji hususani kupitia simu za mkononi na kuongeza ushiriki wa watanzania katika mfumo jumuishi wa fedha.
Amesema, matumizi ya fedha kidijitali hurahisisha malipo mbalimbali, kuongeza uwazi, kuweka kumbukumbu za malipo na usalama wa fedha za watumiaji.
“Baraza linatambua kwamba mfumo imara na salama wa malipo na miundombinu ya kidijitali ni mojawapo ya nguzo kuu za uchumi wa kidijitali Tanzania ambavyo ni vipaumbele vya serikali katika sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) na katika kuimarisha ustawi wa watanzania.”Amesema Msuya
Kauli ya Msuya imekuja baada ya Bunge la Bajeti kupitisha bajeti kuu ya serikali yam waka wa fedha 2023/2024 na kufuta tozo za miamala ya simu ambayo ilikuwa ukituma na kutoa pesa unakatwa tozo.
Msuya, ametoa wito kwa watumiaji wa huduma za mawasiliano, hasa za fedha kupitia simu za mkononi na mifumo ya kidijitali, kutumia fursa hii ya kuondolewa kwa baadhi ya tozo kufanya miamala kwa uhakika na ufanisi zaidi kwa shughuli zao za kiuchumi, kijamii na kibinafsi.
Msuya, ametoa wito kwa watumiaji kuwa makini wanapotumia mitandao ya simu kufanya miamala ya kifedha au huduma nyingine kulinda namba zao za siri
ili kujihadhari na wahalifu.
“Baraza linapenda kuwakumbusha watumiaji, kutoa taarifa kupitia namba 15040 pindi wanapopata ujumbe wowote wenye kiashiria cha utapeli ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya wahalifu.
“Aidha, tunawaomba watanzania kulinda miundombinu ya mawasiliano na kuunga
mkono jitihada za Serikali kuifanya Tanzania kuwa ya kidijitali.”Amesema
Wakati huo huo, Msuya amesema Baraza wanaipongeza serikali pia kwa uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa minara mipya 758 katika kata 713 Tanzania Bara na 48 katika shehia 38 Zanzibar na kuongeza uwezo na nguvu ya minara 304 katika maeneo mbalimbali nchini.
“Hatua hii itawezesha watumiaji wa simu za mkononi maeneo ya vijijini kupata huduma za intaneti ya kasi na kuongeza wigo wa watumiaji wa huduma za mawasiliano kunufaika na kushiriki katika mapinduzi ya uchumi wa kidijitali.
“Ujenzi na uimarishaji wa miundombinu ya mawasiliano vijijini ni mojawapo ya
mikakati ya serikali kueneza matumizi ya mawasiliano ya kasi kwa wananchi ili
kufikia lengo la kuwezesha asilimia 80 ya Watanzania kutumia intaneti ifikapo 2025,”amesema.