SHINYANGA; MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imewataka watumiaji wote wa mitandao ya kijamii, ambao wamekuwa wakikuta wameunganishwa (tagged) na picha chafu kwenda kutoka taarifa za matukio hayo Jeshi la Polisi.
Mamlaka hiyo hiyo imesema vitendo hivyo ambavyo kwa sasa vimeshika kasi ni kosa kisheria na ni uhalifu kama uhalifu mwingine, ambapo wote waliojikuta wameunganishwa na picha hizo waende polisi kutoa taarifa, ili hatua kali zichukuliwe kwa wahusika.
Kauli hiyo imetolewa na Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa, Mhandisi Imelda Salu, wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari wa Mkoa wa Simiyu, yaliyolenga kuwakumbusha sheria mbalimbali za habari kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Mhandisi Imelda alisema kuwa kwa mujibu wa sheria ya mtandao, ni kosa kisheria kumuunganisha mtu na Picha au taarifa chafu bila ya kuwa idhini yake na kitendo hicho kinahesabika kama uhalifu.
“ Tumeanza kuona vitendo vya mtu kumtag au kumuunganisha na picha chafu mwingine, watu wengi wanalalamika, kama mamlaka tunawaambia walioathirika na vitendo hivyo mamlaka ya kushughulika masuala hayo ni jeshi la polisi hivyo waende watoe taarifa,” amesema Mhandisi.