TCRA yahimiza maudhui ya ndani kwenye tamthiliya, muziki

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imevihimiza vyombo vya habari kuangalia uwezekano wa kutoa nafasi kwa tamthiliya, muziki na michezo zenye maudhui ya ndani ili kulinda utamaduni na nembo ya Taifa.

Akizungumza Dar es Salaam Jumatano kwenye mkutano wa wadau mbalimbali wa vyombo vya habari, sanaa na michezo mwakilishi wa TCRA, Andrew Kisaka alisema tafiti zinaonesha asilimia 80 ya tamthiliya zinazorushwa ni za nje.

Aidha, alisema angalau muziki unaopigwa kwa asilimia 80 umebeba maudhui ya ndani isipokuwa kuna changamoto kwenye ujumbe ulioko ndani yake nyingi zinazungumzia mapenzi kiasi kwamba hakuna kitu ambacho mtu anaweza kujifunza.

“Licha ya kwamba kuna baadhi ya vyombo vya habari vimeanzisha chaneli maalumu kuonesha filamu na tamthiliya za ndani bado hazipewi nafasi kubwa/hazikuzwi sana kama ilivyo kwa zile za nje,” alisema.

Alisema afadhali michezo ya ndani imekuwa na kupewa nafasi tofauti na miaka ya nyuma ambapo kwa sasa mitaani imekuwa ikijadiliwa kila mahali huku akisema kwenye picha jongefu asilimia 80 ni za nje ya nchi, katuni za watoto asilimia 95 ni za nje akihimiza umuhimu wa kutengeneza zenye maudhui yanayoendana na utamaduni wa nchi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui ya TCRA, Habi Gunze alisema sababu ya kuandaa semina hiyo ni baada ya kugundua kuna malalamiko kutoka kwa watumiaji wa vyombo vya habari wakisema tamthiliya zinazorushwa nyingi ni za nje na kutaka itafutwe suluhisho kutoka kwa wadau hao.

Mkurugenzi wa Plus Tv, Ramadhan Bukini alisema changamoto iliyopo maudhui ya vipindi vya ndani kwa mfano ngoma za asili na vingine wanashindwa kurusha kwa sababu picha wanazopokea hazina viwango na ubora utakaovutia huku mdau mwingine kutoka Chanel ten, Albert Kilala akisema kuna gharama za kutengeneza maudhui ya ndani akitaja fedha, rasilimali watu na vifaa kwa ajili ya kuandaa vitu vizuri kwani kunahitajika uwekezaji mkubwa.

 

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button