TCU yaongeza wiki moja kudahili

Katibu Mtendaji TCU, Profesa Charles Kihampa

TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imetangaza kufunguliwa kwa awamu ya tatu ya udahili kwa wanafunzi wa shahada ya kwanza kwa mwaka wa masomo 2022/2023.

Taarifa ya Katibu Mtendaji TCU, Profesa Charles Kihampa ilieleza kuwa udahili huo ungeanza kufanywa juzi hadi Septemba 25.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo kwa umma, awamu ya pili ya udahili kwa ngazi ya Shahada ya Kwanza katika Taasisi za Elimu ya Juu nchini kwa mwaka wa masomo 2022/2023 imekamilika.

Advertisement

Profesa Kihampa alihimiza ambao hawakutuma maombi ya udahili au hawakufanikiwa kudahiliwa katika awamu zilizopita watumie fursa hiyo.

“Tume inaelekeza Taasisi zote za Elimu ya Juu nchini zinazofanya udahili wa Shahada ya Kwanza kuendelea kutangaza programu ambazo bado zina nafasi. Aidha, waombaji na vyuo wanahimizwa kuzingatia utaratibu wa udahili kwa Awamu ya Tatu kama ilivyooneshwa kwenye kalenda ya udahili iliyo katika tovuti ya TCU (www.tcu.go.tz),” alieleza.

Aliagiza waombaji waliodahiliwa katika chuo zaidi ya kimoja katika Awamu ya Kwanza na ya Pili wathibitishe udahili wao katika chuo kimojawapo kuanzia jana hadi Septemba 25.

Profesa Kihampa alieleza kuwa uthibitisho wa udahili unafanyika kupitia akaunti ambayo mwombaji alitumia wakati wa kuomba udahili na kwamba orodha ya majina ya waombaji waliodahiliwa katika chuo zaidi ya kimoja imewekwa kwenye tovuti ya TCU (www.tcu.go.tz).

Alieleza kuwa waombaji udahili wa shahada ya kwanza wanakumbushwa kuwa masuala yote yanayohusu udahili au kujithibitisha katika chuo kimoja yawasilishwe moja kwa moja kwenye vyuo husika.