TCU yasitisha udahili Chuo Kikuu Mwanza

TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imesitisha udahili na usajili wa wanafunzi wa shahada ya udaktari wa binadamu kwa mwaka wa masomo 2025/26 katika Chuo Kikuu cha Mwanza, kutokana na chuo hicho kukiuka masharti ya uwezo wa kudahili.
Akizungumza leo mkoani Mwanza, Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa, alisema uamuzi huo umefikiwa baada ya kubainika kuwa chuo hicho kilipokea wanafunzi wengi zaidi ya uwezo wake wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia, ikiwemo idadi ya wahadhiri.
Kwa mujibu wa Profesa Kihampa, chuo hicho kilipaswa kudahili wanafunzi 60 pekee kama ilivyoidhinishwa na TCU, lakini kilichukua wanafunzi mara 10 zaidi ya idadi hiyo na kushindwa kufanya marekebisho licha ya kupewa maelekezo mapema. “Hatua inayofuata ni chuo kuwapatia wanafunzi hao vibali vya kuhamia katika vyuo vingine vilivyoruhusiwa kudahili wanafunzi wa programu ya udaktari wa binadamu,” alisema.
Ameongeza kuwa wanafunzi ambao watataka kubadilisha mwelekeo wa masomo, watachaguliwa kujiunga na programu nyingine zinazopatikana katika vyuo watakavyohamishiwa. SOMA: TCU yaongeza muda udahili, yafungua dirisha awamu ya 3
Profesa Kihampa alisema chuo kitawajibika kukamilisha taratibu zote za uhamisho kabla ya msimu wa udahili kufungwa, ikiwemo kuwapatia wanafunzi nauli za kuwafikisha vyuoni watakakohamishiwa, wakati taratibu za kurejesha gharama walizolipia zikiendelea. “Kwahiyo chuo hakitaruhusiwa kudahili wanafunzi wapya wa programu ya udaktari wa binadamu kwa mwaka wa masomo 2025/26, badala yake kitaendelea na wanafunzi wa mwaka wa pili na wa tatu,” alibainisha.
Wakati huohuo, Tume imetangaza kuunda kamati maalumu ya wataalam itakayochunguza masuala yote ya kitaaluma chuoni hapo, ili kuruhusu TCU kuchukua hatua stahiki za kuhakikisha chuo kinafuata sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji wa elimu ya vyuo vikuu.



