Tegete mbaroni akidaiwa kulawiti mvulana

JESHI la Polisi Mkoa wa Iringa linamshikilia, Drive Tegete (23) mkazi wa Kijiji cha Kidamali, Kata ya Nzihi wilayani Iringa kwa tuhuma za kumlawiti mvulana wa miaka nane.

Taarifa iliyotolewa na Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa, Issa Suleiman imeeleza kuwa mtuhumiwa huyo alimrubuni mtoto huyo wakati akicheza mpira na wenzake kisha akampeleka katika shamba la mahindi na kutekeleza unyama huo kisha akamuacha na kuondoka zake.

Alisema mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa wakati jeshi hilo likiendelea kukamilisha uchunguzi wa tukio hilo.

Aidha Kamanda ameeleza mafanikio ambayo jeshi lao limepata baada ya kufikisha mahakamani kesi za ubakaji na ulawiti.

Aliyataja mafanikio hayo kuwa ni pamoja na watuhumiwa Ayubu Msigwa na Baraka Mwinuka kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kukutwa na hatia ya makosa ya ubakaji.

Aidha alisema mtuhumiwa mwingine Emanuel Gwandu amehukumiwa kifungo cha maisha jela na kulipa fidia ya Sh Milioni moja baada ya kukutwa mahakamani na hatia ya kulawiti.

Alimtaja mtuhumiwa mwingine kuwa ni Wilbert Yesiga aliyefungwa miaka mitano jela baada ya kukutwa na kosa la kuua bila kukusudia.

Habari Zifananazo

Back to top button