MAMLAKA ya wanyamapori nchini imezindua programu tumizi ya bure inayoruhusu watumiaji wa simu za mkononi kufuatilia kuonekana kwa mamalia adimu ili kusaidia mamlaka kuwalinda.
Programu tumizi hiyo iitwayo ‘Mamalia Atlas Kenya’ au ‘Makenya’, huruhusu mtumiaji yeyote anayemwona mamalia wa mwitu kumtambua na kuweka mahali alipo.
Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, kumekuwa na ugumu katika kuwalinda mamalia hao kwani mabadiliko ya hali ya hewa na shughuli za kibinadamu zinaathiri makazi yao ya asili.
Mtafiti katika Makavazi ya Kitaifa ya Kenya, Dk Simon Musila, alisema kutokana na hali hiyo, Makumbusho ya Kitaifa ya Kenya, Kamati ya Mamalia ya Mazingira ya Kenya na washirika wengine walitengeneza programu hiyo ya simu, ambayo pia hutoa njia ya kupakia picha na maelezo, kama vile idadi ya mamalia wanaoonekana na maeneo yao kamili.
Alisema: “Unaweza pia kuongeza tabia… Ukimwona huyu mnyama anafanya nini? Wanapumzika? Wanakimbia? Wanakula? Wanafanya nini sasa hivi unaowaona?”
Musila alisema ni muhimu kushirikisha umma kwa kutumia teknolojia kusaidia idadi ndogo ya wataalamu wa mamalia waliopo nchini.
Mamlaka ya wanyamapori ilisema wafanyakazi wataweka rekodi za mabadiliko ya mazingira ya wanyama na hali ya maisha.
“Kuna haja ya kuleta watu wengi wanaoweza kuchangia data nyingi,” alisema na kuongeza: “Hawa ni watu kama waongoza safari, watu kama wanafunzi, watalii, watu wanaotoka nje na kukutana na wanyama na watakuwa tayari kuwasilisha data.”
Watumiaji wa programu hiyo ya Makenya, tayari wameripoti zaidi ya kuonekana kwa mamalia 2,500 tangu programu kuzinduliwa Agosti.
Kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali, Afrika inachangia kwa kiasi kidogo katika mabadiliko ya hali ya hewa, lakini inabeba mzigo mkubwa wa matokeo yake.
Makamu wa Rais wa Wakfu wa Wanyamapori wa Afrika, Dk Philip Muruthi, alinukuliwa katika mazungumzo na Sauti ya Amerika (VOA) akisema kuzaliana kwa mamalia adimu na kiwango cha kuishi cha watoto kinapungua.