Tehama yaongeza kasi, yaokoa fedha Mahakama
UTEKELEZAJI wa miradi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), umesaidia Mahakama ya Tanzania kuongeza kasi ya utoaji haki na kusaidia kuokoa fedha.
Ipo mifumo ya Tehama inayotumika katika shughuli za uendeshaji mashauri mahakamani na utoaji haki ukiwemo wa kuendesha kesi kwa njia ya video unaoiwezesha mahakama kuharakisha mfumo wa utoaji haki.
Mfumo huo umewezesha serikali kuokoa zaidi ya Sh bilioni 2 kwa mwaka tangu uanze kutumika katika mahakama kadhaa na magereza nchini yaliyowekewa mifumo ya teknolojia hiyo.
Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020/2025 inaelekeza serikali kuwekeza kutekeleza mradi wa haki mtandao.
Kwa mujibu wa ilani hiyo, serikali inapaswa kuimarisha matumizi ya tehama katika utoaji wa huduma za kisheria na upatikanaji wa haki.
Ilani inaeleza kuwa lengo la mradi huo ni kuunganisha taasisi zote za utoaji haki ikiwemo magereza katika mfumo wa kielektroniki ili kuongeza ufanisi, kuharakisha upatikanaji haki na kupunguza gharama za upatikanaji wa huduma hizo.
Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano wa mwaka 2021/2022 hadi 2025/2026, umegusia na kuhamasisha matumizi ya tehama katika sekta ya utoaji haki na kusisitiza ufanisi wa utoaji haki kwa kuunganisha taasisi za utoaji haki katika mifumo ya tehama.
Waziri wa Katiba na Sheria, Damas Ndumbaro alisema bungeni Dodoma kuwa taasisi sita kati ya 10 zinazohusika na utoaji haki zimeimarisha matumizi ya tehama ili kuweza kushirikiana katika kutoa haki kwa haraka na wakati.
Alizitaja taasisi hizo kuwa ni Mahakama, Ofisi ya Kabidhi Wasii Mkuu, Tume ya Utumishi wa Mahakama, Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma alipozungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria alisema Mahakama ya Tanzania kwa sasa inatumia mifumo ya tehama kurahisisha kazi.
Mifumo hiyo ni pamoja na mikutano kwa njia ya video inayowakutanisha watu na kuwawezesha kutekeleza majukumu bila wahusika kulazimika kukutana ana kwa ana.
Teknolojia hiyo pia imewezesha kuendeshwa mashauri bila washitakiwa kupelekwa mahakamani sanjari na kuendesha mafunzo kwa watumishi na wadau wengine.
“Mfumo huu umesimikwa katika vituo vya mahakama na pia katika baadhi ya magereza. Kwa mwaka 2021 pekee, jumla ya mashauri 17,979 yalisikilizwa kwa kutumia mfumo huu. Matumizi ya mfumo huu yanakadiriwa kuokoa kiasi cha shilingi 2,750,092,736 za Kitanzania kwa mwaka kwa upande wa Magereza, Mawakili, Mahakama na wadau wengine,” alisema.
Katika kipindi cha Oktoba, 2019 Mahakama ya Tanzania iliokoa Sh milioni 129 kwa kuendesha mashauri kwa mfumo wa video ambapo Sh milioni 95 zilikuwa ni kutokana na mashauri na vikao mbalimbali vilivyoendeshwa katika Mahakama ya Rufani na Sh milioni 34 ziliokolewa kutokana na mashauri yaliyoendeshwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Profesa Juma alifafanua kwamba gharama kutumia mfumo huo ilikuwa shilingi milioni 5 ambayo ilihusisha gharama za intaneti pamoja na usafiri wa watumishi kwa ajili ya kwenda kuratibu mfumo huo. Gharama hizo pia zilijumuisha kuwalipa Mawakili wa kujitegemea wanaotakiwa kuwawakilisha wafungwa walio magerezani kwa makosa ya mauaji.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba, Temi Kilekamajenga alisema matumizi ya Tehama yamesaidia kuongeza kasi ya umalizaji wa mashauri.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Wilbert Chuma alisema serikali iko katika makakati wa kusambaza mifumo ya teknolojia ya video katika mahakama ambazo hazina mifumo hiyo.