Teknolojia 3G yaingia Misenyi
SERIKALI imesema kufikia Machi 2023 serikali imekamilisha ujenzi wa minara 13 na inatoa huduma katika teknolojia ya 2G na 3G.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia, Mhandisi Kundo Mathew, wakati akijibu swali la Mbunge wa Nkenge, Frolent Kyombo aliyetaka kujua ni lini serikali itaongeza minara au kuboresha mawasiliano katika kata zote 20 za Wilaya ya Misenyi.
Akijibu swali hilo kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia, Mhandisi Kundo amesema kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imetekeleza miradi ya mawasiliano iliyokamilika katika kata 10 za Wilaya ya Missenyi.
“Kupitia mradi wa Tanzania ya Kidijitali Serikali imeshapata watoa huduma wa kufikisha huduma za mawasilioano katika Kata za Bugorora, Kasambya, Mutukula na Kakunyu, ambapo tayari zimeshapata watoa huduma,” amesema Mhandisi Kundo.