SERIKALI imesema teknolojia ya mawasiliano ya 5G itakuwa na manufaa kwenye sekta za kiuchumi na kijamii nchini na kuiwezesha nchi kuwa na uchumi wa kidijiti.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alisema hayo Alhamis Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa teknolojia hiyo ya Kampuni ya Simu za Mkononi ya Vodacom Tanzania.
Nape alisema Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi chache Afrika zenye teknolojia ya 5G ikitanguliwa na Botswana, Misri, Ethiopia, Gabon, Kenya, Lesotho, Madagascar, Mauritius, Nigeria, Senegal, Shelisheli, Afrika Kusini, Uganda na Zimbabwe.
Alisema Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kujenga mazingira rafiki kwa maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano kwa kuwa mawasiliano yanachangia kutatua changamoto katika jamii na kuchangia nchi kufikia malengo yake.
Nape alisema teknolojia hiyo itanufaisha Watanzania kupitia sekta za nishati, madini, kilimo, ujenzi na viwanda, afya, elimu, usafiri na usafirishaji na kuongeza kasi katika utoaji wa huduma za serikali mtandao.
“Sote tunafurahi kuona nchi yetu imepiga hatua kubwa sana, tumeingia katika orodha ya nchi chache duniani ambazo zimepiga hatua kubwa katika maendeleo haya ya Tehama (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano), Tanzania na sisi leo tumo,” alisema Nape.
Alisema teknolojia ya 5G itaongeza ufanisi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwa kuwezesha watumiaji kufikia kasi ambayo ni mojawapo ya malengo makuu ya serikali katika uwekezaji katika mkongo huo.
Alisema Rais Samia Suluhu Hassan ameishukuru Kampuni ya Vodacom kwa kuiweka Tanzania katika ramani ya Afrika kutokana na kuleta mapinduzi ya kiteknolojia na kuifanya kuwa taifa la kidijiti.
“Sambamba na Tanzania ya kidijiti, serikali imedhamiria kuboresha maisha ya watu na kutengeneza fursa za ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla,” alisema Nape aliyemwakilisha Rais Samia.
Alisema kizazi cha sasa kina bahati ya kushuhudia maendeleo ya teknolojia ambayo wengi wao wasingeweza kufikiria kwamba ingeweza kuwafikisha walipo sasa.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Vodacom Tanzania, Jaji mstaafu Thomas Mihayo alisema kampuni hiyo inafurahi kufanya kazi na serikali na kuahidi kuwa itaendelea kutoa ushirikiano katika kujenga taifa la kidijiti.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Vodacom Tanzania, Hilda Bujiku alisema kampuni hiyo imedhamiria kuunganisha Watanzania katika mtandao kwa viwango vya kimataifa pamoja na kuendelea na mpango wa kuboresha mawasiliano mijini na vijijini.