Teknolojia ilivyowarahisishia wakulima shughuli zao

SAYANSI na Teknolojia imewawezesha wakulima kuondoka kwenye mfumo wa kizamani wa kunyunyizia viuatilifu kwa mabomba ya kubeba mgongoni hadi utumiaji wa akili bandia kwa kutumia ndege nyuki.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Profesa Joseph Ndunguru amesema hayo alipozungumza na HabariLeo wakati wa Kongamano la mifumo ya chakula Barani Afrika linaloendelea mkoani Dar es Salaam.

“Sayansi na teknolojia ndio msingi mkubwa wa maendeleo ya uchumi wananchi yoyote kwa mfano wakulima wetu kwa muda mrefu wamekuwa wakitumia teknolojia ya zamani kwa kunyunyuzia viuatilifu kwa mabomba ya kubeba mgongoni lakini sasa hivi kwa kutumia akili bandia tunakuja na matumizi ya ndege nyuki ambayo yatafanya hii kazi ya kunyunyizia viuatilifu,” amesema.

Amesema kwa teknlojia hiyo ya ndege nyuki waliyonayo katika mamlaka hiyo, ndege nyuki moja inaweza kubeba lita 40 za viuatilifu ambayo inanyunyiza shamba la hekta 21 kwa saa ambayo ni sawa na eka 52.

Amesema pia utumiaji wa teknolojia katika kilimo unawezesha kutambua aina ya wadudu waliopo katika mmea husika ambao ndege nyuki hiyo wakati wa unyunyizaji wa kiuatilifu inapuliza kwenye visumbufu hivyo hivyo vilivyolengwa na kiuatilifu husika.

“Kama unataka kupulizia mimea yenye wadudu aina fulani ndege nyuki itaenda kufanya upulizaji kwenye mimea ile tu yenye hao wadudu na sio mingine hiyo inapunguzia gharama kwa mkulima lakini inaenda kuleta tija kubwa,” alisema.

Amesema pia vipo vifaa ambavyo vinatumika kuchunguza vinasaba vya mdudu kwa kuelewa aina ya mdudu husika ili aweze kunyunyiziwa kiuatilifu ambacho ni sahihi kitakachomdhibiti.

Amesema matumizi mengine ya sayansi na teknolojia katika kilimo yatawezesha kuwadhibiti wafanyabiashara wasio waaminifu na kutolea mfano kwa mtu anayechukua mchele nchi ya Thailand, lakini akadanganya na kusema ni wa Mbeya ili kukwepa kodi, ikiwekwa kinasaba chake kwenye hicho kifaa itasema ukweli wa ulipotoka huo mchele.

Akizungumzia kongamano hilo amesema mifumo ya chakula Barani Afrika inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi, ongezeko la watu kwa hiyo changamoto hizo zinasababisha kushuka kwa uzalishaji hivyo jukwaa hilo ni maalum kwa kuwa linakutanisha wadau mbalimbali pamoja.

“Lengo ni kujadili mikakati mikubwa ambayo inahusisha matumizi makubwa ya sayansi, teknolojia na ubunifu ili kuja na suluhu katika kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo. Lengo ni kuboresha tija lakini pia lishe pamoja na soko,” amesema.

Amesema wadau hao wamekutana kutafuta suluhu ya mageuzi katika sekta ya kilimo kwani asilimia 60 ya ardhi duniani inayofaa kwa kilimo inapatikana Afrika, mpaka kufikia mwaka 2020 watu milioni 580 Afrika walitegema kilimo kwa chakula lakini pia ajira.

Amesema pamoja na yote hayo mchango katika sekta ya kilimo katika ukuaji wa uchumi ni kidogo.

Habari Zifananazo

Back to top button