Teknolojia kusambaza Kiswahili

CHAMA cha Lugha na Fasihi ya Kiswahili Tanzania (CHALUFAKITA) kimetakiwa kutumia teknolojia katika kukuza na kusambaza lugha ya Kiswahili katika sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Ombi hilo limetolewa leo na Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma wakati wa kongamano la sita la kimataifa la CHALUFAKITA liliozinduliwa leo jijini Mwanza.
“Nawapongeza sana Chalufakita kwa kuweza kuwaunganisha wadau mbali mbali wa Kiswahili. Ni wakati sahihi sasa kwa Chalufakita kutumia mifumo ya teknolojia katika kukuza lugha ya Kiswahili” amesema Mwinjuma.
Katika hatua nyingine,Mwinjuma ameviagiza vyuo vikuu nchini kuandaa mitaala ya kufundishia ya lugha ya Kiswahili.
Amesema serikali ipo katika hatua za mwisho za kuboresha sera ya utamaduni ya mwaka 1997 haswa katika kipengele cha lugha.
Mwinjuma amepongeza juhudi za Rais Samia katika kukuza lugha ya Kiswahili. Ameweka wazi kuwa Serikali ya Tanzania na Chuo cha Harvana nchini Cuba wapo katika mpango wa kuanza kufundisha Kiswahili katika chuo hicho na lugha hiyo itaanza kufundishwa Oktoba, mwaka huu.
Mwenyekiti wa Chama cha Lugha na Fasihi ya Kiswahili Tanzania(CHALUFAKITA) Dk Mussa Hans amesema wataendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuendeleza Kiswahili kwa kutumia mfumo wa Tehama.
Amesema mada kuu ya kongamano mwaka huu ni Nafasi ya Kiswahili kitaifa na kimataifa.
Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Simon Sirro amesema katika nchi ya Zimbabwe shule nyingi za watu binafsi zinaomba Kiswahili ianze kufundishwa katika shule hizo.
Amesema mpaka sasa nchini Zimbabwe kuna madarasa mawili yanayofundisha lugha ya Kiswahili katika miji ya Bulawayo na Harare.