Teknolojia uzalishaji, mbolea zina tija ulimaji mtama

MATUMIZI sahihi ya mbegu bora, teknolojia za uzalishaji zilizo bora pamoja na matumizi ya mbolea vinaongeza tija katika ulimaji wa zao la mtama ambalo linakabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Kituo cha Tumbi mkoani Tabora, Dk Emmanuel Mrema amesema hayo katika maonesho ya Kitaifa ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi yanaoendelea katika Viwanja vya John Mwakangale mkoani Mbeya.

Dk Mrema ambaye pia ni mgunduzi wa mbegu hasa za mtama amesema zao hilo ni mkombozi kwa mtanzania na serikali ndio maana watafiti wanafanya kazi kubwa kuhakikisha wakulima wanapata mbegu zilizo bora.

“Pili wakulima wanapata teknolojia za uzalishaji bora wa mtama ikiwemo matumizi sahihi ya nafasi, matumizi ya mbolea pia uvunaji kwa wakati kuondoa changamoto ya upotevu wa mazao baada ya kuvuna.

“Hii yote inakwenda ili kutatua changamoto ya mabadiliko ya tabia ya nchi kwenye maeneo mengi ambapo unakuta mbegu za mahindi na mazao mengine hayawezi kufanya kazi tunapolima mtama basi uvunaji unakuwa ni mzuri,” amesema.

Ameongeza kuwa kutokana na viini lishe vingi vilivyopo katika zao hilo wamekuwa wakiwahamasisha watu kutumia zao hilo.

“Ukiangalia afya za watu wanapata matatizo mengi ya kiafya lakini viini lishe ambavyo vipo vingekuwa na uwezo mkubwa wa kutatua hizo changamoto na tukiangalia sasa hivi soko la mtama ni kubwa ndani ya nchi na nje ya nchi,” amesema.

Amesema kwa Tanzania mtama unatumika viwandani, lakini ni chakula kinachotumiwa na watu wengi, pia majani yake baada ya kuvuna hutumika kwa mifugo.

“Kuna kila sababu ya kutoa uhamasishaji mkubwa wa wakulima kulima mtama lakini na kuwaunganisha wakulima waweze kupata masoko ya ndani ya nchi na nje ya nchi, tunapozunguza nje ya nchi tunaangalia Sudani wanatumia sana mtama, Uganda wanatumia sana mtama hizi nchi zote jirani wana matumizi makubwa ya mtama,” amesema.

Amesema pia wanaangalia ni jinsi gani mkulima anaweza kuchanganya mtama na vyakula vingine vikaboresha afya yake.

“Unakuta mtu anachanganya mtama na mahindi, anachanganya mtama na udaga unaotokana na mihogo, kwa hiyo vyote hivi tunamwezesha mkulima aweze kulima kwa wingi na walaji waanze kutumia kwa wingi,” amesema.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dk Geofrey Mkamilo ameeleza kuwa jukumu kubwa la taasisi hiyo ni kutafiti, kusimamia, kuhamasisha na kuratibu shughuli za utafiti nchini.

Na kwamba taasisi hiyo imegundua teknolojia mbalimbali za aina mbalimbali za mbegu bora, mbinu za kilimo bora na ubunifu.

Amesema teknolojia hizo haziko vituoni bali wamezipeleka kwa wakulima kuwajulisha kwa mfano wa mbegu kwenye mazao tofauti tofauti.

Habari Zifananazo

Back to top button