KATIKA kumuenzi Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, Makumbusho ya Taifa, imewahimiza Watanzania kutembelea maeneo mbalimbali ya makumbusho kujifunza kazi mbalimbali zilizofanywa na Nyerere wakati wa uhai wake.
Miongoni wa mambo yaliyopo Makumbusho ya Taifa, Dar es Salaam ni gari la mwisho lililotumiwa na Mwalimu Nyerere kabla ya kufikwa na mauti, ambalo lilimpeleka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa, Dar es Salaam, kueleka hospitali ya St. Thomas Uingereza kwa matibabu, ambako alifariki dunia Oktoba 14, 1999.
Mhifadhi wa Makumbusho hiyo, Pius Gondeka, amesema gari hilo, aina ya Mercedes Benz E 300, limetengenezwa Ujerumani na kununuliwa na serikali ya Tanzania, Desemba 17, 1996.
Amesema gari hiyo imetumiwa na Mwalimu Nyerere katika shughuli m balimbali hususani katika Jiji la Dar es Salaam, baada ya kustaafu.
Amesema gari hiyo ni ya mwisho kutumiwa na Mwalimu Nyerere kipindi cha uhai wake.
“Kwa mara ya mwisho gari hyo ilitumiwa na Mwalimu Agosti 31, 1999 alipotoka nyumbani kwake Msasani kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere tayari kwa safari ya London, Uingereza kupata matibabu,” amesema.
Amesema Baba wa Taifa alifariki Oktoba 14,1999 nchini Uingereza na Septemba 24, 2004 mjane wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere aliitoa gari hiyo kwa Makumbusho ya Taifa.
Gondeka amesema gari nyingine ni Mercedes-Benz 230.6, ilitumika katika shughuli za serikali, wakati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ilipoanza mwaka 1967 na kuvunjika mwaka 1977 kwa sababu mbalimbali.
Amesema upekee wa gari hilo ni kuwa liliweza kubeba marais wawili kwa wakati mmoja, Makamu wa Rais na mwandishi wa Rais ina sehemu tatu kwa ndani.
Amesema ni gari ambayo pia ilikuwepo nchini Kenya na hata Uganda, iwapo viongozi wa nchi hizo walitembelea nchi nyingine kwa shughuli za EAC walitumia gari hiyo na kwamba gari hiyo ilipelekwa Makumbusho Oktoba 2002.