TIMU ya soka ya taifa kwa watu wenye ulemavu, Tembo Warriors, imefanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia baada ya kuifunga Japan mabao 3-1 katika hatua ya 16 bora Istanbul nchini Uturuki jana.
Mabao ya Tembo Warriors yalifungwa na Salim Chambo, Shedrack Hebron kabla ya Japan kujifunga. Tembo inayonolewa na Salvatory Edward, ilionesha soka safi na ukomavu kwenye dakika 50 za awali za mechi hiyo, ambapo matokeo yalikuwa 1-1 kabla ya kuongezwa dakika 20 za ziada na Tembo kuongeza mabao mawili.
Kwa ushindi huo, Tembo inasubiri mshindi wa mchezo mwingine uliotarajiwa kupigwa jana baina ya Marekani na Haiti kwa ajili ya kukutana naye robo fainali kwenye mechi itakayopigwa leo.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa na Katibu Mkuu wake, Dk Hassan Abbasi waliongoza kutoa hamasa na mikakati ya ushindi wakiungana na Watanzania waishio nchini humo. Mchengerwa akizungumza baada ya ushindi huo alisema timu hiyo imeonesha uzalendo mkubwa kilichobaki ni kumalizia kutwaa kombe.
Timu zingine zitakazokutana katika robo fainali Angola dhidi ya Brazil, Morocco inamsubiri mshindi kati ya Mexico dhidi ya Uturuki, ambao ndio wenyeji wa michuano.
Robo fainali nyingine itazikutanisha Uzbekistan dhidi ya Italia. Italia ikifuzu baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Iran.