WAKALA wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA) imeahidi kushirikiana na wadau mbalimbali kutoa mafunzo kwa mafundi wa magari na vivuko kutoka Temesa.
Hayo yamesemwa leo mkoani Mwanza na Meneja wa Temesa Mkoa wa Mwanza, Gilly Chacha wakati wa semina ya siku moja kwa mafundi magari na vivuko kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa. Semina hiyo iliandaliwa na kampuni ya Total Energies.
“Mafunzo haya yatawasaidia sana mafundi wetu na hii ni kutokana na soko la magari limevamiwa sana na kuna wachakachuaji wanatengeza vilainishi feki.” amesema Chacha
Amesema Temesa itaendelea kusimamia matumizi sahihi ya vilainishi. Alisema kupitia mafunzo hayo mafundi wamejengewa uelewa wa kuweza kugundua ni aina ipi ya mafuta na spea zipi na kwenye gari lipi vifaa hivyo vinatakiwa kuwekwa.
Amesema tangu Temesa iingie mkataba mwaka 2022 wa uletewaji mafuta na Total Energies imewasaidia sana kuondokana na wimbi la uchakachuaji wa mafuta.
Mwakilishi kutoka Total Energies Julius Magele amesema semina kwa mafundi ni muhimu sana na hiyo imetokana na kubadilika kwa teknolojia.
Magele amesema mafunzo hayo yamewasaidia mafundi kuongeza ufanisi katika utendaji wao wa kazi.
Amesema kumekuwa na changamoto kubwa sana ya mafundi wengi kufanya kazi kwa mazoea jambo linalopelekea magari kuharibika mara kwa mara. Amesema tatizo lingine ni mafundi wamekuwa wakichanganya vilanishi katika magari.
Naye fundi kutoka Temesa Mwanza,Rashid Hussein ameomba mafunzo kwa mafundi yawe endelevu ili mafundi kuongezewa uelewa na kuendana na teknolojia.