Ten Hag: Rashford hauzwi
MANCHETER, England: KOCHA wa Manchester United, Erik ten Hag amesema mshambuliaji wake Marcus Rashford hauzwi licha ya tetesi za kutakiwa na klabu tajiri ya Ufaransa, Paris St-Germain (PSG).
Ripoti za awali zilieleza kwamba PSG wangetoa ofa ya pauni milioni 75 kwa Rashford huku nyota wao Kylian Mbappe akiondoka kwenda Real Madrid baada ya msimu huu lakini kocha huyo amedai Rashford ameshaanza mazoezi kamili kwa ajili ya michezo ijayo.
Katika kukatisha tamaa zaidi Ten Hag ameweka wazi kwamba Rashford ni sehemu ya mipango yake ya muda mrefu katika klabu hiyo ya Man United na ameshasaini mkataba wa miaka minne zaidia wa kuitumikia klabu hiyo hadi 2028.
“Hatukumpa mkataba mpya wa miaka minne kwa lengo la kumuuza, hapana! Tuna mipango naye ya muda mrefu yeye ni sehemu ya mradi wa Man United,” ameeleza Ten Hag.
Rashford anatarajiwa kurudi mchezoni dhidi ya Liverpool kesho katika robo fainali ya Kombe la FA. Kasi yake inaweza kuwa nyenzo muhimu kwa United kama atarudi akiwa timamu.
PSG inatafuta washambuliaji badala ya mshambuliaji wake nyota Kylian Mbappe kuhusishwa na Real Madrid ya Hispania.