KIONGOZI wa Equatorial Guinea, Teodoro Obiang Nguema Mbasogo amechaguliwa tena kuwa rais kwa muhula wa sita akipata asilimia 94.9 ya kura zilizopigwa, maafisa wa uchaguzi walitangaza siku ya Jumamosi.
Wagombea wawili, Andrès Esono Ondo na Buenaventura Monsuy Asumu, kila mmoja alipata takriban 9,700 na 2,900 kati ya kura 413,000 nchini Equatorial Guinea.
Mkuu wa tume ya uchaguzi Faustino Ndong Esono Eyang alithibitisha kuwa Obiang atahudumu kwa miaka saba katika wadhifa huo. Tume hiyo imesema waliojitokeza kupiga kura katika uchaguzi huo ni asilimia 98.
Obiang, 80, ambaye alichukua mamlaka katika mapinduzi ya 1979, ndiye mkuu wa nchi aliyeongoza kwa muda mrefu zaidi duniani bila kujumuisha wafalme.
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 80 amekuwa madarakani kwa miaka 43 utawala mrefu zaidi wa kiongozi yeyote aliye hai ulimwenguni leo isipokuwa wafalme.