TET mguu sawa mtaala mpya

DAR ES SALAAM. Siku moja baada ya Serikali kutangaza kukamilisha mapitio ya Sera mpya ya Elimu na Mafunzo, Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), imesema imekamilisha kuandaa vitabu vya kiada na ziada kwa ngazi zote.

Sera ya Elimu na Mafunzo imefanyiwa mabadiliko kwenye maeneo kadhaa ikilinganishwa na sera iliyopita kwa kuongeza fursa za elimu ya amali (elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi) ambayo itaanza kutolewa kuanzia kidato cha kwanza.

Mkurugenzi Mtendaji wa TET, Dk Aneth Komba leo Novemba 3, 2023 ameiambia HabariLEO kuwa  kazi ya kuandaa vitabu vya kiada katika Ngazi za Elimu ya Awali, Msingi na Sekondari, kwa ajili ya matumizi kwa madarasa yatakayoanza kutekeleza mtaala mpya mwaka 2024 imeshamilika.

“Tumejipanga na tunakamilisha kazi ya kuidhinisha vitabu vya ziada ili navyo viwe tayari mapema kabla ya mwaka wa masomo kuanza,” amesema.

Jana Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitangaza kuwa serikali imekamilisha mapitio ya sera ya elimu na inaandaa taratibu kuizindua.

Majaliwa alisema hayo bungeni Dodoma wakati anatoa taarifa kuhusu uidhinishwaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Toleo la 2023 na Mitaala ya Elimu Ngazi ya Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Elimu ya Ualimu.

“Serikali inaendelea na maandalizi ya kuanza kwa utekelezaji wa sera na mitaala iliyoidhinishwa kwa kuzingatia kalenda ya utekelezaji wake,” alisema.

Majaliwa alisema mitaala iliyoidhinishwa imejikita katika kuwajengea wanafunzi ujuzi stahiki kwa ajili ya soko la ajira na imetoa kipaumbele kwa stadi za amali katika kila ngazi ya elimu.

Alisema Sera ya Elimu na Mafunzo imefanyiwa mabadiliko kwenye maeneo kadhaa ikiwa ni pamoja na elimu ya lazima kuwa ya miaka 10 badala ya saba kama ilivyo sasa.

“Aidha, elimu hiyo ya lazima inajumuisha elimu ya msingi ya miaka sita, elimu ya sekondari ya chini ambayo itatolewa kwa miaka minne,” alisema Majaliwa.

Aliongeza: “Utekelezaji wa pendekezo hili utaanza kufanyika mwaka 2027 sambamba na kufuta mtihani wa darasa la saba na badala yake kuanza kufanyika kwa tathmini darasa la 6 kwa ajili ya kujiunga na elimu ya lazima ya sekondari.”

Majaliwa alisema pia sera mpya imezingatia kuongeza fursa za elimu ya amali (elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi) ambayo itaanza kutolewa kuanzia kidato cha kwanza.

 

Habari Zifananazo

3 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button