DSM; TAASISI ya Elimu Tanzania (TET) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wamesaini hati ya makubaliano ya kushirikiana kikazi katika maeneo saba.
Lengo la ushirikiano huo ni kutokana na maoni ya wadau wa elimu kutaka somo la kupinga rushwa liingizwe katika mitaala ya elimu na kuwajengea uzalendo watoto, ili kupunguza vitendo vya rushwa. Mitaala hiyo itaingizwa katika shule za msingi, sekondari na vyuo vya kati.
Akizungumza leo Oktoba 18, 2023 Mkurugenzi wa TET, Dk Aneth Komba amesema lengo la ushirikiano huo unaendana kwa ukaribu na majukumu ya TET, ambayo ni kubuni na kukuza mitaala katika ngazi za elimu ya awali, elimu ya msingi, sekondari na vyuo vya ualimu.
Kutoa mafunzo kwa walimu tarajali na walio kazini ili kuleta ufanisi na matokeo bora ya utekelezaji wa mitaala, kutoa na kuhakiki udhibiti wa ubora wa elimu unaohusu mbinu za ufundishaji, malengo ya masomo na viwango vya zana za kufundishia na kujifunzia
Majukumu mengine ni kutoa ushauri wa kitaalamu kwa serikali kupitia Wizara na wadau wa elimu unaolenga kuboresha elimu katika ngazi mbalimbali.
“Ushirikiano umekuja wakati muafaka wakati tunakamilisha kazi ya kupitia mitaala, kuingiza maboresho katika mitaala yetu kwa ngazi ya awali, msingi, sekondari na vyuo vya kati,” amesema.
Ameyataja maeneo saba ambayo watashirikiana na Takukuru ni kutoa mafunzo kwa timu ya wakuza mitaala wa TET juu ya masuala ya kuzuia na kupambana na rushwa.
“Wakuza mitaala tunawaita ‘academic staff’ hawa ndio wanaoshiriki katika zoezi zima la kuandaa mitaala na kuandika vitabu, ni imani yetu wakuza mitaala hawa wakipata mafunzo, wataweza kuingiza vizuri masuala ya kuzuia na kupambana na rushwa katika mitaala na katika vitabu,”amesema Dk Komba
Amesema pia Takukuru wataandaa na kuwasilisha TET maudhui mbalimbali ya kuzuia rushwa, na masuala hayo yatachopekwa kwenye vifaa mbalimbali vya ufundishaji na ufunzaji, ikiwemo vitabu, miongozo na maudhui ya kielektroniki kwa shule za awali, msingi, sekondari na vyuo vya uwalimu.
“Niwashukuru Takukuru wameweza kutuletea maudhui ambayo tumeyaingiza katika rasimu za vitabu, tutawaita mje kuangalia vizuri yaliyoingizwa kwenye mitaala, lengo ni kuleta mabadiliko kwa watoto, ”amesema Dk Komba.
Amesema Takukuru na TET watatoa mafunzo kwa walimu na waandishi wa vitabu vya ziada kuhusu masuala ya kupambana na kuzuia rushwa, kuwapatia vifaa ili waweze kufikia lengo.
Pia amesema Takukuru na TET wataunda kamati ya kutathmini na kuangalia utekelezaji na namna ya kuboresha, ikiwemo kubadilishana taarifa za kuzuia rushwa kwa waandaji wa mitaala.
Kwa upande wa Mkurungezi wa Takukuru, Salum Hamduni amesema katika kuzuia vitendo vya rushwa, Takukuru imekuwa ikitekeleza jukumu hilo kwa mfumo usio rasmi kwa kufikia makundi vya vijana kupitia uelimishaji kwa kuanzia klabu za wapinga rushwa katika shule ya msingi, sekondari na vyuo vya kati
–
Amesema, kwa mujibu wa takwimu walizonazo hadi Juni 2023 jumla ya klabu 10,736 zenye wanachama milioni 1.91 zimeanzishwa katika shule za msingi.
Na klabu za wapinga rushwa katika shule za sekondari ni 4,390 zenye wanachama 398,340 ambapo kwa vyuo vya kati ni 84 wanachama 2462 zimeanzishwa katika vyuo na taasisi za elimu ya kati na elimu ya juu.
“Takukuru tunaamini endapo elimu ya maadili na mafunzo dhidi ya rushwa yataanza kuwafikia Watanzania wakiwa bado kwenye umri mdogo, vita dhidi ya vitendo vya rushwa vitapungua kwa kiwango kikubwa;…… Kwa sababu vijana watakuwa katika maadili na kujua rushwa ni nini na madhara yake na namna gani wanaweza kushiriki katika mapambano.
“Katika hili ni lazima tuwapandikizie uzalendo, utii na kujiamini katika kushiriki kwa kuona rasilimali za umma zinatuhusu sisi sote,”amesema Hamduni.
Comments are closed.