DAR ES SALAAM: WALIMU wametakiwa kuwapa wanafunzi mbinu mbali mbali za kuwajenga na kujitambua katika ujibuji wa maswali.
Agizo hilo limetolewa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) leo Machi 7, 2024 katika mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo walimu wa Shule ya Msingi Buguruni kuhusu Maboresho ya Mtaala Mpya, ikiwa ni kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kesho Machi 8,2024.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Mtunza Mitaala kutoka TET, Blandina Francis amesema ni vema walimu wakatoa nafasi ya pili kwa mwanafunzi pale anapomuuliza swali ili aweze kujielezea kwa ufasaha.
“Sio Mwalimu unamuuliza swali mwanafunzi akajibu kwa kukosea unasema mwingine…, pale humjengi mtoto, yamkini jibu la mwanzo amejibu kwa kiwewe ndio maana amekosea, mpe nafasi nyingine zaidi ajielezee,”amesema Blandina na kuongeza
“ Walimu sio Kisiwa cha Maarifa hata Mwanafunzi anapaswa kuachiwa aseme kile anachokifahamu, kuwa mwalimu haimanishi kuwa unajua kila kitu;….. “Wanafunzi wapewe mbinu mbali mbali ili waweze kujitambua anapoulizwa swali mpe nafasi ya kujieleza hata kama amekosea mpe nafasi nyingine.”amesisitiza Blandina.
TET wametoa mafunzo ya Maboresho ya Mtaala Mpya kwa walimu wa Shule ya Msingi Buguruni kwa siku mbili ambapo jana waliwafundisha walimu namna ya kuandaa mandalio ya masomo na mitihani pamoja na mbinu mbali mbali za ufundishaji na leo wamewasimamia walimu hao kuwafundisha wanafunzi kwa vitendo.
Nae, Mwalimu Ramadhani Ally wa shule hiyo anayefundisha darasa la tatu akizungumza amesema, baadhi ya changamoto zilizokuwa zinawakabili zimeboreshwa ikiwemo mbinu za ufundishaji darasani na kukabiliana na dhana tata wanazokumbana nazo kuhusu Mtaala huo Mpya.
“Changamoto kubwa iliyokuwa inatukabili ni ni namna ya kuandaa somo na maandalizi ya ufundishaji, pia maudhui yaliyopo kwenye mitaala mipya kwa baadhi ya masomo kama Sayansi tulikuwa tunaona umahili uliopo upo juu ukilinganisha na ‘level’ ya mwanafunzi wa darasa la tatu, hata hivyo TET wametushauri tuwafundishe wanafunzi umahili huo kulingana na ‘level’ yao na mazingira halisi mwanafunzi aliyopo.
“Tumeingia darasa na kufanya kwa vitendo tukifuata maalekezo, tumeweza kujifunza kwa mifano halisi kutokana na mazingira,”amesema.
Kwa upande wa Mwalimu Happines Sahiba amesema amefurahishwa na namna ya kufanya maandalizo ya masomo na mitihani na mbinu mbali mbali walizopewa za kuwafundisha wanafunzi kujitambua.