DAR ES SALAAM: Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo imetoa maelekezo mawili kwa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kutoa taarifa ya utekelezaji wa Mtaala wa elimu nchini.
Kamati hiyo ya Kudumu imetoa maagizo hayo ilipofika katika Taasisi hiyo kujionea namna inavyotekekeza majukumu yake ambapo hadi kufikia Machi 2024 tayari imepokea asilimia 97 ya bajeti iliyotengewa kwa Mwaka wa Fedha 2023/24
Akitoa maagizo hayo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Husna Sekiboko amesema TET inapaswa kutoa na kusimamia utekelezaji wa mitaala mipya nchi nzima ili mwanafunzi anapohitimu aweze kujiajiri na sio kusubiri kuajiriwa.
Pia, wameitaka TET kuhakikisha uwiano wa vitabu kwa wanafunzi unakuwa sawa yaani kitabu kimoja kwa motto mmoja na sio kitabu kimoja kwa watoto watatu kama ilivyo sasa.
“Siku za nyuma ilikuwa lundo la wanafunzi wanatumia kitabu kimoja, mnyonge mnyongeni TET mmefanya kazi kubwa ya kuhakikisha sasa uwiano wa kitabu ni watoto watatu kitabu kimoja, hata hivyo tunawaagiza hakikisheni mnazalisha vitabu vya kutosha kila mwanafunzi awe na kitabu chake.
“Na hili linawezekana sio kwamba haliwezekani, mbona shule za binafsi kila mtoto ana kitabu chake, kama bajeti haitoshi wekeni malengo leteni bajeti yenu tutawapitishia.”amesema Husna.
Aidha, Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda akizungumza amesema wamepokea maelekezo hayo ya kamati na watayatekeleza.
Awali akizungumza Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dk Aneth Komba amesema kazi ya uandishi na uchapaji wa mitaala, mihtasari, vitabu vya kiada na Viongozi vya Mwalimu kwa Darasa la kwanza, tatu na kidato cha nne mkondo wa Amali imekamilika.
Dk Komba amesema fedha hizo zimewezesha uandishi wa vitabu vya kiada kwa madarasa yanayotekeleza mtaala mpya, ununuzi wa vifaa vya kuchapa vitabu vya kiada vya wanafunzi wenye mahitaji maalum pamoja na kutoa mafunzo kwa walimu kuhusu mtaala mpya.
Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa usambazaji wa nakala laini za vitabu hivyo umefanyika kupitia Maktaba Mtandao ya Taasisi hiyo pamoja na kuchapa nakala zaidi ya milioni nane vya kimacho , maandishi yaliyokuzwa na Breli kwa ajili ya wanafunzi wenye uoni hafifu na wasioona na kwamba usambaji hadi sasa umefikia asilimia 64
Aidha, Dk Komba amesema kwa upande wa mafunzo kwa wasimamizi na watekelezaji wa mitaala mipya yamefanyika katika makundi matano ambayo ni pamoja na wawezeshaji wa kitaifa, wasimamizi wa utekelezaji, walimu wa elimu ya awali juu ya maudhui na ufundishaji wa somo la English na pia kwa walimu wa Sekondari Mkondo wa Amali wa shule zote 96 zilizoanza kutoa mafunzo hayo.
Ameongeza kuwa taasisi hiyo inaendelea kufanya tathimini na ufatiliaji wa utekelezaji wa mitaala ili kubaini changamoto na kutoa afua stahiki za kuimarisha utekelezaji wa mitaala hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo kazini kwa walimu na wasimamizi wa utekelezaji wa mitaala kazi ambayo inaendelea kupitia Mpango Endelevu wa Mafunzo ya Walimu Kazini (MEWAKA)