HUALIEN, Taiwan: TAKRIBANI watu tisa wamefariki dunia, huku 1,067 wakijeruhiwa baada ya tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 7.4 katika kipimo cha Richter kutokea katika eneo la Hualien nchini Taiwan.
Shirika la Zimamoto nchini humo (NFA) limesema zaidi ya watu 663 wamekwama kwenye vifusi na wengine 42 hawajulikani walipo kutokana na tetemeko hilo.
Maofisa wa nchi hiyo wamesema tetemeko hilo ndilo lenye nguvu zaidi kuwahi kutokea katika nchi hiyo katika kipindi cha miaka 25. Huku tetemeko hilo likileta tahadhari za kutokea kwa mafuriko ya sunami yanayokadiliwa kufika kwa mataifa ya Japan na Ufilipino.
Maofisa hao wamesema tetemeko hilo wakati linatokea mashariki ya kisiwa cha Hualien idadi kubwa ya watu walikuwa katika shughuli za uchimbaji wa migodi. Vikosi vya uokoaji vinajaribu kuwafikia walionasa.
Eneo la Hualien linakadiriwa kuwa na wakazi zaidia ya watu 300,000 kati ya watu milioni 23 wanaoishi nchini Taiwan.
Tetemeko hilo lilifuatiwa na mitetemeko mikali ya baadae, ikijumuisha tetemeko la ukubwa wa 6.4. Mitetemeko mingi ya inatarajiwa kutokea siku zijazo.