TFF yaipiga faini Simba Sh milioni 2
BODI ya Ligi (TPLB) imeipiga faini ya Sh milioni 2 klabu ya Simba SC katika matukio mawili tofauti yanayohusu michezo yake ya Ligi Kuu.
Kosa la kwanza la faini ya Sh milioni 1, Simba imepigwa faini hiyo kwa kosa la mashabiki wake kumwaga vitu vyenye asili ya unga katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi kabla ya wachezaji hawajaanza kufanya mazoezi siku moja kabla ya mchezo dhidi ya Tabora United.
Tukio hilo limetafsiriwa kama vitendo vinavyoashiria imani za kishirikina jambo ambalo ni kinyume na matakwa ya kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu udhibiti wa klabu.
Taarifa iliyotolewa leo Februari 15, 2024 na Shirikisho la Mpira wa Miguu ( TFF) imeeleza kuwa pia Simba imetozwa faini nyingine ya Sh milioni 1 kwa kosa la mashabiki wake kuingia katika eneo la kuchezea ‘pitch’ baada ya mchezo dhidi ya Azam FC uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
TFF wameeleza kuwa adhabu hiyo ni kwa kuzingatia kanuni ya 17:60 ya Ligi Kuu kuhusu taratibu za mchezo.